HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2019

LIPULI YAILIPUA YANGA 2-0

 Mashabiki wa Lipuli FC wakishangilia timu yao baada ya kuifunga Yanga bao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) katika mchezo uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa. (Picha na Tullo Chambo).






NA MWANDISHI WETU, IRINGA

WANA Paluhengo Lipuli FC, wamekatiza ndoto za Yanga kuwania tiketi za kuiwakilisha nchi Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC), baada ya kuwachapa mabao 2-0, katika nusu fainali Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).

Hii ni mara ya pili kwa Lipuli kuifyatua Yanga katika Uwanja wa Samora mjini hapa mwaka huu, baada ya Machi 16, kuzaibua bao 1-0, lililofungwa na Haruna Shamte, katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Wabishi hao Iringa, walitinga fainali ya ASFC baada ya kuibuka na ushindi huo kwenye Uwanja wa Samora mjini hapa, na sasa wanaenda kuumana na Azam FC katika fainali kali kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi, hapo Juni 2.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Shomary Lawi wa Kigoma, mabao ya Lipuli yalifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Paul Nonga dakika ya 27 na Daruwesh Saliboko dakika ya 38, na kudumu hadi filimbi ya mwisho.

Mchezo huo ambao uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa, Yanga iliuanza mpira kwa kasi na kukosa nafasi za kufunga mabao, lakini safu yao ya ushambuliaji ilikuwa butu.

Licha ya mwanzo huo wa Yanga, Lipuli walicheza kwa umakini na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa Nonga ambaye alimaliza mpira uliotemwa na kipa wa Yanga, Klaus Kindoki, kufuatia shuti kali la Saliboko.

Kuingia kwa bao hilo, kuliiongezea nguvu Lipuli, ambao walicharuka na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 37, likifungwa Saliboko, akitumia vema makosa ya Kindoki ya kuutema mpira alioanza kupiga yeye mwenyewe na kuukwamisha nyavuni.

Licha kufanya mabadiliko mbalimbali kwa timu zote mbili, lakini hayakuleta tija na Lipuli iliyokuwa chini ya Kocha, Samwel Moja na Suleiman Matola waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutinga fainali.

Kwa matokeo hayo, Yanga inaelekea kuwa mtazamaji wa michuano ya klabu Afrika msimu ujao, kwani licha ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), wana nafasi finyu ya kuwapoka mahasimu wao Simba taji hilo wanalolishikilia.

Na kipigo hiki kinakuja siku mbili baada ya kuchaguliwa kwa uongozi mpya wa klabu chini ya Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla na Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela, waliochaguliwa juzi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Pilisi, Oysterbay, Dar.

Katika uchaguzi huo, wagombea waliochaguliwa katika nafasi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Hamad Islam, Mhandisi Bahati Mwaseba, Dominick Ikute, Kamugisha Kalokola, Arafat Haji, Salum Ruvila, Saad Khimji na Rodgers Gumbo.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Lipuli FC, Matola alisema anashukuru vijana wake wamefanya kile walichokuwa wamepanga, ambacho ni kucheza fainali ASFC ilikusaka tiketi ya kucheza kimataifa.
Alisema fainali hiyo dhidi ya Azam FC itakuwa ngumu kutokana na ubora waliokuwa nao, lakini wanafungika, na kwamba wataenda Lindi kushinda mechi hiyo.

Kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kipindi cha kwanza beki yake ilicheza ovyo ndio maana wameadhibiwa.
Alisema kwa walipofika wanashukuru kwani msimu huu hawakuwa na malengo ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu wala Kombe la Shirikisho ASFC.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, uwanjani liliibuka shangwe kwa mashabiki wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kasesela, huku milio ya woh! woh! Who ikianikiza, wakiigiza kama Mbwa.

Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Yusuph Mohammed, Haruna Shamte, Paul Ngalema, William Lucian ‘Gallas’, Ally Sonso, Freddy Tangalu, Miraj Athumani ‘Madenge’/Novaty Lufunga, Jimmy Shoji, Paul Nonga, Dariwesh Saliboko na Zawadi Mauya/Steven Maganga.

Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Mwinyi Hajji/Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vicent ‘Dante’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’/Amissi Tambwe, Heritier Makambo, Papy Tshishimbi na Ibrahim Ajib/Juma Abdul.

No comments:

Post a Comment

Pages