Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa (kulia), akizindua rasmi matumizi ya Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Jijini
Dodoma, wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Na Josephine Majura na Peter Haule,
WFM, Dodoma
Kiwango cha umaskini nchini Tanzania kimepungua kwa
asilimia mbili, ikiwa ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya
kupunguza umasikini kwa wananchi hasa wa hali ya chini.
Hayo
yamebainishwa wakati Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa, akizindua ripoti ya matokeo ya viashiria muhimu vya
utafiti wa mapato na matumizi ya mwaka 2017-18 na jengo la Ofisi ya Taifa ya
Takwimu, Mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa, amewataka Watakwimu nchini
kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo mbalimbali
wakati wa kutekeleza majukumu yao hususan kuzalisha na kusambaza takwimu
zenye viwango vya kitaifa na kimataifa ili kuisaidia
Serikali kujua mahitaji yaliyopo.
“Serikali
inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inatambua umuhimu
wa takwimu zenye ubora, kwa kuwa ndiyo
macho na masikio ya Serikali katika kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo
ya nchi”, alieleza Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa, alisema kuwa takwimu bora hutoa
fursa kwa Serikali kufanya mapitio ya sera, mipango na mikakati kulingana na
hali ilivyo kwa wakati husika na pia kupima ilikotoka, ilipo na kutabiri inakoelekea
hivyo kupima mwenendo wa jitihada za Serikali.
Aidha
aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu Nchini (NBS), kuhakikisha Halmashauri zote
nchini zinakuwa na Afisa Takwimu ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu kwa
wakati ili kuweza kusaidia maendeleo nchini.
Kwa
upande wake Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Wizara
yake imepewa jukumu la kusimamia Uchumi wa Taifa, lakini haiwezi kusimamia
uchumi bila kuwa na takwimu rasmi na sahihi.
“Katika
kipindi cha takribani miaka mitatu na nusu tangu Serikali ya Awamu ya Tano
iingie madarakani, umaskini nchini umepungua hadi kufikia takribani asilimia 26
kutoka asilimia 28, ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia mbili”, alisisitiza
Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa matokeo
ya tafiti yaliyozinduliwa na Mhe. Kassim Majaliwa, yameonesha kupungua kwa
umaskini wa watanzania waishio vijijini kwa asilimia 3.1 kati ya mwaka 2011/12
na mwaka 2017/18.
Alieleza
kuwa hayo ni matunda ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano, chini ya Kiongozi wake, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli.
Kwa
upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa, alisema kuwa utafiti
wa mwaka 2017/2018 umetumia teknolojia ya kisasa inayojulikana kama Survey Solution ambayo ni tofauti na
njia ya awali ya kutumia madodoso yaliyochapishwa hivyo kupunguza gharama za kufanya
tafiti za kijamii.
Wawakilishi
wa Mashirika ya Kimataifa akiwemo Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Denis Biseko,
wameipongeza Serikali kwa kupunguza kiwango cha umasikini kwa takribani
asilimia 2, na pia wamepongeza matokeo ya utafiti huo ambao umezingatia usawa
wa kijinsia hivyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwa ni moja ya lengo la
mashirika hayo.
No comments:
Post a Comment