HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 06, 2019

Wanawake: TASAF imeokoa ndoa, familia zetu

Baadhi ya wanawake walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi (TASAF), kutoka Kijiji cha Kibaoni, Wilaya ya Singida Vijijini mkoani Singida, wakizungumza na baadhi ya waandishi na maofisa wa TASAF.


NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

WANAWAKE walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya Maskini zaidi (TASAF), wamesema ndoa zao zimeimarika baada ya kufanikiwa kiuchumi kutokana na biashara wanazofanya.

Wakizungumza na baadhi ya maofisa wa TASAF na waandishi wa habari waliotembelea miradi inayotekelezwa na walengwa hao kwenye vijiji vya Wilaya ya Singida Vijijini, walisema fedha kidogo wanazopata kwenye mpango huo wanazitumia kuanzisha miradi midogo.

Farida Rajab Kim wa Kijiji cha Kibaoni Kata ya Mudida, alisema hivi sasa heshma imerudi kwenye familia yake baada ya kumudu kufanya biashara ya mboga mboga, kuku, mbuzi na kujenga nyumba ya bati kupitia malipo ya kazi za muda kwenye miradi ya TASAF na ruzuku anayopokea kila baada ya miezi miwili.

"Ukiwa huna hela wanakudharau mume wangu alikuwa ananiona Mimi mzingo maana kula yetu ilikuwa ya kuvizia, watoto hawaendi shule maana hawana sare wala madaftari.

"Nimeingia TASAF nikapewa Sh. 20,000 nikafundishwa namna ya kuitumia kibiashara nikanunua kuku watatu na iliyobaki nikaenda kulangia nyanya na mboga za majani," alisema Kim.

Kwa mujibu wa mlengwa huyo tangu 2014 alivyoingia TASAF hadi sasa watoto wake wanne wanaenda shule vizuri, familia yake ina uhakika wa milo mitatu, amejenga nyumba ya bati 24 na biashara zake zinaendelea huku akisisitiza kwamba amejiunga kwenye kikundi cha kuweka na kukopa.

Akieleza namna alivyookoa ndoa yake, Hajra Jumanne alisema ufukara aliokuwa nao ulimfanya akatengwa na ndugu huku mume akimtelekeza na watoto wanne.

"Sikufikiria kulala kwenye kitanda, chakula kilikuwa cha kubabaisha watoto hawaeleweki lakini ulipokuja mpango wa TASAF, huwezi kuamini maisha yamebadilika kabisa, najiona mtu katika watu.

"Wanangu wanakwenda shule wasafi, tunao uhakika wa milo mitatu na matunda... biashara yangu ya pombe inaendelea kwa mtaji wa Sh. 30,000 nilizopewa kwenye mpango huu. Nimewekeza mabati dukani yamefika 16 nataka yafike 30 nimeanza kujenga nyumba ya tofali za kuchoma.

"Sasa hivi mume wangu ananiambia nakupenda mke wangu ananisaidia kuwa andaa watoto waende kule na wakati mwingine namnunilia nguo mapenzi yamerudi familia yetu sasa imekuwa bora," alisema Jumanne.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini, Pitazis Tindikali, alisema kila mlengwa wa mradi huo anapewa elimu sahihi ya ujasiriamali mdogo ili kujiongezea kipato na kuondoka chini ya mstari wa umaskini.

"Hatugawi fedha tunawaambia tunawapa mbegu tu waifanyie kazi kwa kuwa mpango huu ukifika ukomo watalazimika kutoka na kuwaachia wengine. Tumewasaidia kujiunga kwenye vikundi huko wanajifunza kutunza fedha zao, wanakopeshana na kufanya biashara ndogo," alisema Tindikali.

No comments:

Post a Comment

Pages