Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza Mkuu
wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (kushoto), wakati wa mkutano wa kusikiliza
kero za ardhi kwa wananchi wa Iringa kupitia programu ya Funguka kwa Waziri
katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo uliopo Manispaa ya Iringa jana. Katikati ni
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Waziri wa Adhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini
kuanza kujitathmini katika idadi ya hati za ardhi wanazotoa kwa wamiliki wa
ardhi kwenye halmashauri zao.
Alisema Wizara yake
itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika Upangaji, Umilikishaji na Utoaji
Hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini hamashauri ambazo ziko nyuma katika kutoa
hati za ardhi kwa wananchi.
Lukuvi alisema hayo jana katika
mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa mkoa wa
Iringa kupitia programu ya Funguka kwa Waziri uliyofanyika ukumbi wa Siasa ni
Kilimo katika Manispaa ya Iringa,
‘’Mkurugenzi ajione
fahari kuwaezesha wananchi kwa kupima na kuwapatia hati, kama Mkurugenzi huwezi
kutoa hati miliki hata mia moja basi wewe hufai’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kumilikisha
na kumpatia mwananchi hati ya ardhi ni kumuwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza
kuitumia hati kwenye shughuli za kimaendeleo na kusisitiza kuwa wakurugenzi wa
halmashauri wahakikishe wanapanga na kuwamilikisha maeneo wananchi.
Aidha, Lukuvi alisema kwa
sasa wizara yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma za ardhi karibu na
wananchi kwa kuanzisha ofisi za mikoa zitakazokuwa na watendaji wote wa sekta ya
ardhi kama vile Wapimaji, Wathamini, Wataalamu wa Mipango Miji pamoja na Wasajili.
‘’Sasa Wapimaji,
Wathamini na Wapangaji watakuja hapa Iringa, muundo unaanza mwezi ujao lengo ni
kuwapunguzia usumbufu wananchi katika kupata huduma za ardhi’’ alisema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi alisema, katika kuboresha huduma za sekta ya ardhi, Wizara
yake itatumia mifumo unganishi itakayorahisisha utendaji kazi kwa wataalamu wa
sekta ya ardhi ambapo kazi kubwa itakuwa ikifanyika kielektroniki badala ya
kutumia makaratasi aliyoaeleza kuwa wakati mwingine husababisha tamaa kwa
maafisa ardhi.
Alitolea mfano mkoa wa
Dar es Salaama kuwa, ushaanza kutumia mfumo unganishi ambapo sasa wamiliki wa
ardhi katika mkoa huo wanapatiwa hati za kielectroniki na kubainisha kuwa lengo
la kuwa na mfumo unganishi ni kuondoa urasimu na kurahisisha utendaji kazi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa
Ally Hapi alieleza kuwa mkoa wake umejitahidi kupunguza kero na migogoro ya
ardhi iliyokuwepo miaka ya nyuma kwa kuanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi
kwenye maeneo yao kupitia programu ya Iringa Mpya.
Alimueleza Waziri Lukuvi
kuwa, kama angekuja mwaka mmoja na nusu uliopita basi ukumbi aliofanyia mkutano
wa Funguka kwa Waziri ungekuwa umejaa wananchi wenye kero za ardhi lakini
jitihada za mkoa wake zimesababisha mkutano huo kutokuwa na idadi kubwa ya wananchi
wenye migogoro ya ardhi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
‘’Muda mwingi nautumia
kwenda kwa wananchi na kazi za ardhi zina changamoto kubwa na njia pekee ya kukabiliana
nazo ni kutenda haki bila kujali uwezo, kabila ama dini ya mtu’’ alisema Hapi.
No comments:
Post a Comment