Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Dk. Ashatu Kijaji, akizungumza wakati akifungua
Kongamano la Kumi la Waatalamu wa Ununuzi
na Ugavi (PSPTB), ambapo aliagiza wachukuliwe hatua wale wote waliopelekwa
kwenye Baraza la Maadili kulingana na uzito wa makossa yao ili taaluma hiyo
iendelee kufanya kazi kwa weledi, Jijini Dodoma. (Picha na Josephine Majura WFM – DODOMA).
Na
Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dk. Ashatu Kijaji, ameiagiza Bodi ya Manunuzi na Ugavi kuwachukulia
hatua waliopelekwa kwenye baraza la maadili
kulingana na uzito wa makosa yao ili taaluma hiyo iendelee kufanya kazi
kwa weledi bila rushwa.
Agizo hilo limetolewa
Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa 10 wa Wataalamu wa Ununuzi na ugavi kutoka maeneo mbalibali nchini.
Dkt. Kijaji alisema
kuwa, kuna ununuzi usiozingatia sheria na kanuni na kusababisha kununua bidhaa
zilizo chini ya kiwango, ununuzi hewa wa huduma na bidhaa na kutokuwepo kwa
kumbukumbu za ununuzi na mikataba hewa licha ya uwepo wa wataalam hao.
“Mamlaka ya Udhibiti
wa Manunuzi wa Umma kwa mwaka 2018/19 inaonesha mikataba 12 kutoka taasisi tisa
za umma yenye thamani ya shilingi bilioni 25.8 ina viashiria vya rushwa kwa
kuwa utaratibu wa manunuzi kwa mikataba hiyo haukufuatwa”, alieleza Dk. Kijaji
Alisema kuwa taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha kuwa ununuzi wa
jumla ya Sh. bilioni 16.6 haukuwa kwenye bajeti wala mpango wa ununuzi
ulioidhinishwa na Sh. bilioni 24.85 zimetumika kulipa mikataba ambayo haikuwa
na hati ya utekelezaji.
Dkt. Kijaji amewataka
waajiri wote kutoa ushirikiano kwa bodi za kitaaluma hususan linapojitokeza
suala la usimamizi wa maadili kwa wataalamu waliosajiliwa na bodi husika, kwa
kuwa hakuna ufanisi bila maadili.
Aidha Dk. Kijaji,
ameupongeza uongozi wa PSPTB kwa hatua zilizochukuliwa za kusimamia mahitaji ya
ajira ya kada ya ununuzi na ugavi kwa kuwapeleka mahakamani watu wanaofanya
kazi za ununuzi na ugavi bila kuwa na sifa stahiki.
Hivyo akawataka
waajiri wote kuhakikisha wanaajiri watumishi wenye sifa zinazotambuliwa na
PSPTB na kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye waraka wa Maendeleo ya utumishi wa
mwaka 2015.
Naibu Waziri Dk.
Ashatu Kijaji, ameiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kufanya
tathmini ya uwezo na uadilifu wa taasisi za umma zilizobeba dhamana ya ununuzi
Serikalini.
Alielekeza kuwa
taarifa ya Baraza la Maadili iwasilishwe wizarani mapema ili iweze kupitiwa na
kufanya maamuzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali.
Amesema kuwa Wizara
ya Fedha na Mipango itaendelea kuunga mkono juhudi za Bodi zinazolenga kuondoa
kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi, kwa kuwa
bajeti ya ununuzi wa Serikali ni takribani asilimia 80 ya bajeti yote.
Kwa upande wake
Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma, Dk. Fredrick Mwakimbinga,
alisema kuwa Bodi inafanya jitihada za dhati kuhakikisha taaluma ya ununuzi na
ugavi inatoa mchango unaotarajiwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kulingana
na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano, ili kutimiza malengo hayo bodi imetoa
mafunzo mahususi kwa taasisi mbalimbali ambayo yameongeza ufanisi katika
taasisi husika.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfrey Mbanyi, amesema kuwa Bodi hiyo imeahidi kufanyia
kazi maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Dk. Kijaji. Amebainisha kuwa licha
ya kuwa na Sheria inayowataka watumishi wanaofanya kazi ya ununuzi na ugavi kusajiliwa,
bado wapo ambao hawafanyi hivyo, Bodi itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa
wale wote watakao kiuka sheria.
No comments:
Post a Comment