Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua jengo la Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar, baada ya kuweka jiwe la msingi la hoteli hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mradi wa ujenzi wa hoteli ya Golden Tulip
Airport Zanzibar ni muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii na
huduma za malazi kwa wageni wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amani Karume.
Amesema
mradi huo unakwenda sambamba na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar za kuimarisha uwanja wake wa ndege ili kuongeza uwezo wake
katika kutoa huduma bora kwa abiria na wafanyakazi wa mashirika ya ndege
ya ndani na nje ya nchi.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 4, 2020), wakati akiweka
jiwe la msingi la ujenzi wa hoteli hiyo. Miongoni mwa watakaonufaika na
mradi huo ni pamoja na wasafiri wanaopita Zanzibar kwa ajili ya
kuunganisha ndege na baadaye kuendelea na safari.
Waziri
Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport
Zanzibar inayojengwa katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amani Karume ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 56 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yam waka 1964.
Ujenzi
wa hoteli hiyo unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 8.5. sawa
na sh. bilioni 19.55. “Ama kwa hakika uwekezaji huu ni mkubwa na
naamini wawekezaji hawa wengeliamua kuwekeza katika nchi nyingine
yoyote, nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wangelipokelewa kwa
mikono miwili.”
“Hata
hivyo, mazingira mazuri ya uwekezaji hapa Zanzibar na uzalendo alionao
Mhe. Mohamed Raza, Mwenyekiti wa ‘Royal suites group of companies’
vilipelekea ushawishi mkubwa wa hoteli ya aina hii kujengwa hapa
Zanzibar.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa “Nyote mtakubaliana nami kuwa viwanja vingi vya ndege
vilivyopo kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, havina hoteli kubwa na
za kisasa zilizopo karibu na viwanja hivyo. Uamuzi wa kujenga mradi huu
ni sahihi, kwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni mahali salama na
wezeshi kwa biashara na uwekezaji.”
Amesema
kwa upande mwingine, Serikali zinaendelea kuimarisha amani na utulivu,
miundombinu wezeshi ya kiuchumi, huduma za fedha na mifumo ya kodi ili
kuvutia uwekezaji. “Mambo haya ni muhimu sana katika kuvutia wawekezaji
katika sekta mbalimbali kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”
Hivyo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein
kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya za kushajiisha uwekezaji.
“Tunawashukuru sana.”
Amesema
kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi hiki cha miaka tisa ya Awamu ya
Saba, ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, jumla ya miradi ya uwekezaji
304 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.74 imeidhinishwa na
mingine iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Utekelezwaji
wa miradi hiyo, umetoa mchango mkubwa katika kukuza ajira, teknolojia,
kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha ustawi wa Wananchi wetu.
“Hivyo, nawapongeza wawekezaji wetu wote waliowekeza na wanaoendelea
kuwekeza hapa nchini. Wawekezaji hawa wameonesha imani na upendo mkubwa
kwetu, nasi tunaahidi kufanya nao kazi kwa ushirikiano makubwa.”
Kwa upande wake,
Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi
Mohammed Ramia amesema mradi huo ni muhimu kwa kuwa utakapokamilika
utaenda kuongeza mapato ya Serikali.
Amesema
hoteli hiyo ni ya kwanza kwa Zanzibar kwa sababu mbali ya kuwa na
ukumbi wa watu mashuhuri (VIP Business Lounge) ambao wageni wake
watakuwa na uwezo wa kukamilisha taratibu za abiria wa ndege (check in)
na taratibu za uhamiaji moja kwa moja kutoka katika ukumbi huo.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Royal
Group of Companies, Bw. Hassan Mohammed Raza alisema ujenzi wa hoteli
hiyo yenye vyumba 61, kumbi tatu za mikutano zenye uwezo uwezo wa
kuchukua watu 600 ina hadhi ya nyota nne, ulianza februari 2019 na
unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Alisema
nembo ya Golden Tulip ni sehemu moja ya kampuni ya pili kwa ukubwa
duniani kwa upande wa hoteli ukiwa chini ya mwavuli wa Louvre Hoteli
ambayo inamilikiwa na Shanghai Municipal Council. Mtandao huo una hoteli
zaidi ya 8,000 duniani, hivyo hoteli yao italazimika kufuata na
kutimiza vigezo bora vya hoteli katika sekta ya hoteli duniani.
No comments:
Post a Comment