WALIMU Mkoani Tabora wametakiwa kuwalea kimaadili wanafunzi na wanavyuo
ili waweze kukua katika uadilifu na uzalendo ambao utakaowawezesha kushiriki ujenzi
wa Tanzania mpya msingi mkuu ni viwanda.
Kauli hiyo imetolewa leo na
katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa ufunguzi wa mafunzo
na maelekezo kuhusiana na uendeshaji wa
klabu za maadili kwa walimu wa shule za msingi ,sekondari na vyuo.
Alisema kuwa katika kukuza uchumi Tanzania mpya ipo haja ya kuwa na
vijana ambao wamekuzwa katika msingi ya uadilifu na uzalendo ambao utaweka
mbele maslahi ya Taifa na sio masalahi binafisi.
“Maslahi ya Taifa yatadumu daima …lakini maslahi ya mtu binafsi ni
ya muda baada ya kufa basi nayo yamekwisha” alisema.
Makungu alisema mafunzo hayo ni muhimu sana katika kujenga jamii
yenye maadili mema ambayo yatasaidia kuzalisha Viongozi wazalenda na waadilifu.
Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwapongeza walimu kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya ya
kukuza maadili mkoani Tabora na kuongeza kuwa uanzishwaji wa Klabu za Maadili utaleta mabadiliko chanya na kuongeza ufaulu kwa vijana mashuleni na vyuoni.
Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma Gerald Mwaitebele alisema Ofisi hiyo imeamua
kuanzishia Klabu hizo ili kuwajenga vijana tangu awali ili kuwajenga kukua kimaadili
na uzalendo wakiwa wadogo.
Alisema ni kazi kubwa kufundisha umuhimu wa maadili kwa mtu mzima
kuliko kufundisha akiwa mdogo kwa kuwa atajengeka katika hali ya uadilifu na
kuipenda nchi yake.
Mafunzo hayo ya siku moja
yameshirikisha walimu wa shule za Msingi, sekondari na Vyuo vya Elimu vilivyopo
Manispaa ya Tabora na yalikuwa na mada za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Mgongano wa
Masilahi na Mwongozo wa Uanzishwaji na Uendeshaji wa Klabu za Maadili
No comments:
Post a Comment