Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akijadili jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kabla ya kuanza mkutano kwa njia
ya video na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu
wa Mikoa akiwa ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma, Machi 21, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu
wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia
ya video akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Machi 21, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameonya juu ya upotoshwaji na utoaji holela wa
taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na virusi vya
corona (COVID 19) unaofanywa na watu mbalimbali nchini.
Amesema
kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu
na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha
mikanganyiko.
Waziri
Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumamosi, Machi 21, 2020) wakati akizungumza
na Wakuu wa Mikoa yote nchini, Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga
Wakuu wa Mikoa kwa njia video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini
Dodoma.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
ifuatile watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya
kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Watu
wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona
badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa
hatua,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu amesema licha ya hali ya maambukizi ya corona nchini kutia
matumaini, viongozi hao hawana budi kupeana taratibu za namna ya
kukabiliana na tatizo hilo.
“Wakuu
wa mikoa kila mmoja ahakikishe eneo lake linakuwa salama na endapo
kutakuwa na mgonjwa tumieni zahanati ambazo bado hazijaanza kutumika kwa
ajili ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa corona,” amesema.
Amewataka
wakuu hao wa mikoa waimarishe utoaji wa elimu kwa umma na ikiwezekana
watumie magari ya matangazo ili wananchi waelewe athari za ugonjwa huo
na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu ili waweze kuendelea na
shughuli zao za kimaendeleo.
Pia
amewataka watumie redio za kijamii katika maeneo yao kutoa elimu kwa
umma juu ya kujikinga na ugonjwa huo na wasimamie maeneo ya utoaji
huduma kama vituo vya mabasi na kuhakikisha kila abiria anakaa kwenye
kiti.
“Nendeni
kwenye maeneo ya mikusanyiko, vituo vya mabasi kutoa elimu kwa umma na
kuwaondoa hofu. Upande wa maofisini, viwandani na kwenye mgodi kuwe na
utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyakazi kila siku asubuhi watumie hata
robo saa kabla ya kuanza kazi waelekezwe namna ya kujikinga.”
Waziri
Mkuu amesema kwa wanaoishi katika maeneo ya makambi, viongozi wao
waelekezwe namna ya kutoa elimu ya kujikinga na corona na pia wadhibiti
utorokaji na Serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha udhibiti
mipakani, uwezo wa kupima sampuli na upatikanaji wa vifaa.
Amewataka wakuu hao wa mikoa, wawashirikishe wakuu wa wilaya kwenye mikoa yao ili wasimamie utekelezaji wa maagizo hayo.
Wakati huohuo,Waziri
Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanawafuatilia na
kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaobainika kuongeza bei kwa
bidhaa ambazo zinatumika katika udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa
corona.
Kuhusu
viongozi wa dini, Waziri Mkuu amewaomba waendelee kushirikiana na
Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za
ugonjwa huu. Pia awaendelee kuliombea Taifa.
No comments:
Post a Comment