NA JANETH JOVIN
DAWA za kulevya zikiwemo Kilogram 118.074 za Heroin, Kilogram 3.932 za Cocaine na kilogram 120 za bangi zimeteketezwa jijini Dar es Salaam baada ya kesi zake kumalizika mahakamani.
Zoezi la kuteketezwa kwa dawa hizo lililofanyika leo jijini Dar es Salaam katika kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Wazo Tegeta, limeshuhudiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Edwin Kakolaki Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Biswalo Mganga, wawakilishi mbalimbali kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) akiwemo Kamishna ukaguzi na Sayansi jinai wa mamlaka hiyo Bertha Mamuya .
Akizungumza wakati wa zoezi la kuteketezwa kwa dawa hizo, Jaji Kakolaki amesema wanaziteketeza kwa sababu kesi zake zimekwisha malizika mahakamani.
"Kwa utaratibu uliopo, baada ya kesi za dawa za kulevya kuletwa mahakamani na tukapokea kielelezo cha dawa hizo, kesi ikimalizika mahakama utoa amri ya kuziteketeza na ndicho kilichofanyika leo hapa," amesema
Amesema uteketezaji wa dawa hizo ufanyika kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwamo DPP, DCEA, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mawakili wa kujitegemea na serikali, kwa lengo la kushuhudia.
"ki msingi hawa niliyowataja ni lazima wawepo kushuhudia amri ya mahakama ya uteketezaji wa vielelezo hivyo imefanyika tena kwa uwazi kabisa ili watanzania waweze kujua kesi ikiisha lazima ziteketezwe, na hii inajidhihirisha kuwa maneno ya mtaani kuhusu kwamba dawa hazifanyiwi chochote siyo ya kweli," amesema
Naye DPP, Mganga amesema "Dawa hizo zilizoteketezwa zimetokana na kesi 15 ambapo mwaka jana mwezi Oktoba tuliteketeza Kilogram 10.65 za cocaine na Kilogram 226.149 za Heroin ambazo zilitokana na kesi 17.
"Jumla ya kesi hizo yaani za mwaka jana na leo ni kesi 32 na jumla ya dawa za heroin tulizoteketeza kwa kipindi cha miaka miwili ni Kilogram 345.22 na Cocaine Kilogram 14.58 huku bangi ikiwa kilogram 120, hizi ni kwa mkoa wa Dar es Salaam peke yake" amesema
Hata hivyo amesema kesi iliyokuwa na dawa za kulevya nyingi aina ya Heroin ni iliyohusisha raia Iran ambao wamehukumiwa na Mahakama Kuu Kitengo cha uhujumu uchumi kifungo cha miaka 30 jela.
"Hata hivyo sasa hivi tuliacha kusema dawa hizi zinathamani ya shilingi ngapi maana tuliona tunatoa motisha au kuhamamisha watu kwenda kufanya biashara hiyo, hivyo atuwezi kusema zina thamani kiasi gani bali tunasema zina madhara makubwa kwa binadamu," amesema
Aidha Mganga alitoa wito kwa wananchi waendelee kutoa taarifa ili kesi hizo zifike mahakamani na hatimaye wafikie hatua iliyofikia leo ya kuziteketeza na waliohusika kuhukumiwa.
Kwa upande wake Kamishna Mamuya amesema dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa binadamu hivyo anatoa wito kwa jamii hasa vijana kuacha kuzitumia.
"Wanaotumia dawa za kulevya wengi wao uishia kuwa tegemezi ndio maana tunaendelea kusisitiza kuwa watu hasa vijana waache kabisa kutumika dawa hizi," amesema
No comments:
Post a Comment