Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA
wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos
Santos Silayo amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma kujivunia na
kuhifadhi chanzo cha maji cha Mto Ruvuma kilichopo katika milima ya
Matogoro Manispaa ya Songea.
Hayo
ameyasema Julai 26, 2021 mkoani Ruvuma wakati alipoongoza msafara wa
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja kupanda msitu wa
milima ya Matogoro kwenda kujionea Mapango na Chanzo cha Maji cha Mto
Ruvuma ikiwa ni sehemu ya maazimisho ya Tamasha la Majimaji Selebuka
linalofanyika wilayani Songea.
"Mto
Ruvuma umeubeba Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa umepita katika wilaya zote tano
ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na ni kwa sababu
hii wananchi kwa kushirikiana nasi TFS tunapaswa kuuheshimu na kuulinda
msitu huu wa Matogoro, machifu wote Kusini huku wanafanya hivyo,”
alisema Kamishna Prof. Silayo.
Mhifadhi
Mkuu Kanda ya kusini na Kamanda wa Kanda, Manyisye Mpokigwa anasema
chanzo cha Mto Ruvuma licha ya kuwa ni muhimu kwa wakazi wa mkoa wa
Ruvuma ni kivutio cha utalii kutokana na chanzo hicho kuwa katika mfano
wa kisima kidogo ambacho kimetoa mfereji mdogo wenye kazi kubwa ambayo
huwezi kuongelea katika hali ya kawaida na kueleweka kwa jamii.
Anasema
licha ya udogo wa kisima hicho kidogo ndicho kinachounda mto maarufu
duniani unaoitwa Ruvuma ukiwa na urefu za kilometa zaidi ya 800 na upana
wa kati ya meta 300 hadi 500 kutegemea na eneo lililopo kwa sababu kuna
baadhi ya maeneo mto huo una upana mkubwa zaidi.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja ni miongoni mwa
waliokwenda kutalii milima ya Matogolo: “Hii ni safari yangu ya kwanza
kufika hapa, ila nimefurahi sana kuona mazingira ya hivi. Mazingira
yanavutia, kuna upepo mzuri kileleni na pia kuona chanzo cha mto mkubwa
(Ruvuma), inapendeza kwa kweli, tuitunze misitu yetu na tujenge
utamaduni wa kutalii, kuna raha sana kupanda milima kama hii, mimi
nitaendelea kutumia milima ya TFS kama sehemu ya maandalizi yangu ya
kupanda Mlima Kilimanjaro na niwaase wengine kufanya hivyo.”
.
No comments:
Post a Comment