HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 11, 2021

Wadau wapitia sera ya jinsia Zanzibar

Na Talib Ussi

 Wadau na wanaharakati wa utetezi wa haki za Wanawake, Vijana na Watoto wamefanya utafiti mdogo wa kupitia Sera ya Jinsia na Ujumuishi (Gender and Social inclusions Policy) ya Tume Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya mwaka 2015  ili kuona kama demokrasia imezingatiwa katika mchakato wa Uchaguzi nchini.


Wadau hao ni pamoja na Mtandao wa Jinsia Zanzibar (ZGC), Jumuiya ya  Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuia inayojihusisha na kupambana na Changamoto zinazowakabili Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Jumuia ya Vijana Zanzibar (ZYF) na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) ambapo wamefanyakazi ya kuipitia Sera hiyo na kuona mapungufu mbali mbali ikiwemo kutotekelezeka tangu kuanzishwa kwake Februari, 2015.

Kwa mfano  kifungu kidogo cha pili (2.5) kiimeeleza namna ya ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii, wakiwemo wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu katika mchakato mzima wa uchaguzi ikiwemo ugawaji wa majimbo, elimu ya mpiga kura na mambo yote yanayohusiana na uchaguzi. Lakini utafiti huo umegundua makundi hayo hayakushirikishwa ipasavyo kama ilivyoelezwa kwenye sera.
 
Pia sera hiyo katika kifungu 3.1 (a) imeeleza katika kipindi cha miaka mitano ZEC itatoa  mapendekezao ya kuwanyanyua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika uteuzi wa makamishna wa ZEC. 
 
Tunafahamu kuwa mamlaka ya uteuzi wa makamishna sio ZEC kwa kuwa imeainishwa na katiba ya nchi kwamba mwenyekiti na wajumbe wengine wawili watateuliwa na rais, ambapo kati ya hao lazima mmoja awe jaji na wajumbe wengine wane watatoka katika vyama vya siasa ili kuhakikisha kwamba ZEC inasimamia vyema sera ya jinsia na ujumuishi ilisema kwamba mara kwa mara itakua inapendekeza kufanya marekebisho ya katiba ili masuala ya jinsia na ujumuishi yaingie katika katiba na kuifanya sera hii itekelezeke.

Mwenyekiti  wa Jumuia ya Wanawake wenye  Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) bi Salma Saadat amesema Sera hiyo ni nzuri lakini inahitaji kupangiwa mpango kazi  ili iweze kutekelezeka kwani kipengele kidogo Na 4.1 (C) kinasema siku ya kupiga kura ZEC itaandaa sehemu maalum ya uangalizi wa watoto /kucheza ili kuwawezesha wanawake kushiriki uchaguzi vizuri. lakini ZEC hawajawahi kuandaa eneo hilo katika chaguzi zote zilizopita.

Pia amesema utafiti huo umebaini kuwa kamati ya maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar haina usawa wa kijinsia, kwani ina wajumbe wanawake wanne  kati ya  24 ambao ni sawa na asilimia 16 na haikuwahusisha makundi yote bali wanasiasa tu ndio waliyoingizwa kwenye kamati hiyo kupitia vyama vyao.
 
Vile vile uwepo wa kamati hiyo ni wa muda mfupi, huundwa wakati wa uchaguzi  na uhai wake humalizika mara tu baada ya uchaguzi kwisha  na pia kamati hiyo haijawekewa muongozo wa kushuhulikia malalamiko ya ZEC huivunjwa kamati hiyo.  Wala haina muongozo wa kutatua vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakati wa uchaguzi. 
 
“Kuna wanawake walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wakati wa Uchaguzi lakini hawajui waende wapi kupeleka kesi zao, kwasababu kamati haina mwongozo wa kutatua kesi za mtu mmoja mmoja, kamati inapokea kesi za vyama vya siasa tu kwa mfano kesi ya ACT kuhusu kiongozi wao kupinga kuwapo kwa kura za mapema” “ambapo alituhumiwa kuvuruga amani” Alisema Bi Salma.
 
Aidha Wadau wamependekeza Sera ya jinsia na Ujumisho ya ZEC ipitiwe tena pamoja na kuipangia mpango kazi ili iweze kutekelezeka, wamesema ni vizuri ikawepo kamati ya maadili ambayo shirikishi itakayojumuisha mwenyekiti na mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi. Mwanasheria, Afisa kutoka Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, wajumbe kutoka vyama vya siasa na mjumbe mmoja kutoka jeshi la polisi. Hivyo wadau wamependekeza kuwa ni vyema kukawa na kamati mbili moja ya maadili ambayo pamoja na wajumbe waliyotajwa hapo juu wawemo pia na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama wawakilishi kutoka asasi za kiraia.
 
 Kamati ya pili iitwe kamati ya dhamana/uhusiano ya  vyama vya siasa( Political Party Liason Committee), ambayo itajumuisha wanasiasa kwa asilimia kubwa ili kuangalia,kujadili, kushauri na kupendekeza utendaji mzuri wa usimamizi wa mchakato mzima wa uchaguzi na mwenendo wa vyama vya siasa.
 
Vile vile  katika mapendekezo wadau  wameomba katiba  ya Zanzibar ya mwaka 1984 ifanyiwe marekebisho ili wanawake waweze kuteuliwa kwenye nafasi ya Makamishna wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, kwasababu katiba iliyopo sasa haimlazimishi rais wa Zanzibar kuzingatia usawa wa jinsia wakati wa kuteua makamishna wa Tume hiyo ZEC ambapo kwa sasa ZEC ina kamishna moja tu,  mwanamke kati ya saba, sawa na asilimia 14.


No comments:

Post a Comment

Pages