Meneja wa Kikundi cha K&S ART Vision Rashid Pazi akizungumza na Waandishi wa Habari.
Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
MENEJA wa Kikundi cha K &S Vision kilipo Wilaya Temeke jijini Dar es Salaam Rashid Pazi amewaomba wadau, taasisi na serikali kukipatia kikundi hicho sapoti ya kwenda vijijini kutoa elimu ya namna ya kuepuka migogoro ya wafugaji na wakulima.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Meneja wa Kikundi cha K&S ART Vision Rashid Pazi wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mpango wake wa kwenda kutoa elimu kuhusu migogoro inayosababishwa na wakulima na wafugaji.
Pazi ambaye pia ni mjasiriamali alisema lengo la kwenda kutoa elimu hiyo katika mikoa yenye changamoto ya migogoro ya wafugaji na wakulima kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na usalama tangu kupata uhuru wake mwaka 1961.
Alisema wafugaji na wakulima wamekuwa na migogoro ya mara kwa mara ambayo haina sababu kwa kutoelewana na kwamba wote wanategemeana katika maisha yao ya kila siku.
Pazi alieleza kuwa serikali imekuwa ikifanya mambo mengi kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani hivyo anatimu ya watu zaidi ya 30 ambao wataenda kutoa elimu kwa mfumo wa Igizo mapema Oktoba mwaka huu wakianza na Mkoa wa Morogoro.
" Kilichonishawishi kwenda kutoa elimu ya kuwaelimisha wakulima na wafugaji kuacha migogoro ni kutokana na migogoro hiyo kutokea mara kwa mara katika baadhi ya mikoa hapa nchini. Mimi ni mdau wa kuangalia taarifa ya habari kupitia runinga na baadhi ya mitandao ya kijamii nimekuwa nikiona hili tatizo," alisema Pazi.
Aliongeza kuwa migogoro hiyo zamani haikuwepo na kwamba katika historia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa anasema watu wapendane pasiwe na ubaguzi wa dini, kabila, rangi, ukoo na hata mambo mengine ambayo yanaweza kusababisha machafuko.
Meneja huyo alisema endapo watapata sapoti kutoka kwa wadau, serikali matarajio yao ni kufikisha ujumbe wenye faida kwa Taifa ambao wanaamini wakulima na wafugaji watakuwa wamepatiwa mwarobaini.
Alisema washiriki wa igizo hilo baadhi yao ni wasanii marufu wakimo Ben na Hidaya Jaidi pamoja na vijana waliokuwa mitaani ambao wanavipaji vya kuigiza.
Pia alisema kuwa hivi karibuni wanatarajia kuzindua igizo hilo lenye lengo la kutoa elimu inayohusu migogoro ya wafugaji na wakulima.
Naye Hened Fereji alisena kuwa anaunga mkono juhudi za mume wake kwa kitu ambacho amebuni akiamini kwamba kitaleta mafanikio kwa serikali na kwa jamii.
" Sehemu yoyote pale ukiona mafanikio ya nwanaume ujue kuna mwanamke nyuma yake. Rais wetu ni mwanamke ametushauri tusikate tamaa tuwe mstari wa mbele katika mafanikio ndio maana namuunga mkono mume wangu nami ni mshiriki wa igizo hili," alisema.
Kwa upande wake kijana mshiriki wa igizo hilo Irene Chonya alisema serikali imekuwa ikichukizwa na migogoro ya wafugaji na wakulima wataonesha chanzo cha migogoro hiyo inapoanza hadi kufikia hatua ya kupoteza maisha kwa baadhi yao.
No comments:
Post a Comment