Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) limesema Maadhimisho ya Sherehe za Maulidi yanatarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Kagera yakiambatana na shughuli za kijamii pamoja na uzinduzi wa shughuli za kimaendeleo mkoani humo.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeir na Sheikh wa Mkoa wa Kagera Haruna Abdallah Kichwabuta wakati akitoa taarifa ya kuelekea kufanyika maadhimisho hayo Oktoba 18 na 19 katika Manispaa ya Bukoba mwaka huu ambapo yataambatana na uzinduzi wa mpango wa kimaendeleo wa miaka mitano huku kauli mbiu ikiwa ni Maulidi na Maendeleo.
Sheikh huyo amebainisha kuwa kufanyika kwa Maadhimisho hayo Mkoani Kagera ni Fursa kutokana na kutofanyika muda mrefu katika mkoa huo tangu miaka 34 ilyopita ambapo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 1987.
‘Hadhara hii ya Maadhimisho ya Mtume ni maulidi yanayofanyika Kagera baada ya kukaa muda mrefu sasa baada ya kuzunguka muda Mrefu mikoani ndio inaturejelea wanaKagera na tunatarajia InshaAllah Mgeni Rasmi atakuwa Mkuu wa nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh tunamuomba Mwenyezimungu mambo yawe vizuri kama tunavyotarajia’amesema Skeikh Abdallah
Aidha, Sheikh Haruna amesema kuwa miongoni shughuli za kijamii ni pamoja na jamii kupewa elimu ya umuhimu wa matumizi ya bima za afya na pia elimu ya sensa na makazi huku akitoa wito kwa Waislam nchini kushiriki katika maandalizi ya maadhimisho hayo.
Amesisitiza kuwa kabla ya siku ya Maulid waislamu wa Mkoani Kagera watashiriki pia katika kujitolea damu katika Hospitali ya Mkoa ili kuwasaidia watu wote wenye uhitaji kutakuwa ma mashindano ya visomo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment