HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 05, 2021

NAIBU WAZIRI CHILO AWAONYA WATUMISHI NIDA


 NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wa Mkoa wa Dodoma, leo Novemba 4, 2021, alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo ya Mkoa. Ametoa onyo kali kwa baadhi ya watumishi hao nchini wanaochukua rushwa kwa wananchi wakati wanapowasajili hasa wanapoomba Namba za Utambulisho (NIN) au vitambulisho. Wapili kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Deusdedit Buberwa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

Na Felix Mwagara, MOHA, Dodoma

 

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo ametoa onyo kali kwa baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanaochukua rushwa kwa wananchi wakati wanapowasajili, na endapo watakamatwa watachukulia hatua kali.

Chilo amesema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali nchini ambao wameombwa rushwa na baadhi ya maafisa wa NIDA ili wafanyiwe usajili kwa haraka, au kupewa Namba za Utambulisho (NIN), hivyo watumishi hao utumia uharaka huo kuchukua fedha.

Akizungumza na Watumishi wa NIDA wa Mkoa wa Dodoma, leo, alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi katika ofisi hiyo ya Mkoa, Chilo alisema Rais Samia Suluhu Hassan anataka wananchi wasikilizwe na wahudumiwe kwa weledi bila kuombwa rushwa kwasababu vitambulisho utolewa bure.

“Naomba leo niliseme hili hapa, na agizo hili lifike nchi nzima kwa watumishi wote wa NIDA wenye tabia ya kuwaomba rushwa wananchi wanapofika vituoni kupata huduma, simaanishi nyinyi hapa ndiyo mnaomba fedha, hapana, bali tunazo taarifa japo hatuna uhakika nazo kuwa baadhi ya watumishi wanatabia hizo, na endapo tukiwagundua tutawachukua hatua za kisheria,” alisema Chilo na kuongeza kuwa;

“Tukikugundua kuna mtu anawatoza wananchi fedha ili lengo na madhunumini tu aweze kumpa huduma tutamchukulia hatua za kisheria, ni marufuku, na hata zile fomu za ukiangalia pembeni utakuta imeandikwa haiuzwi maana hakuna huduma inayotolewa kwa NIDA ili watu watoe fedha, hakuna, huduma hizi zinatolewa bure, na ikifika wakati Serikali ikiona kuna haja ya  watu watoe chochote itasema, lakini ni marufuku kumtoza mwananchi fedha ili aweze kupata huduma ya NIDA, aidha ya kitambulisho, kupewa namba, hakuna haki inayonunuliwa kwa fedha.” 

Aidha, Chilo aliwataka watumishi wa NIDA kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo kwa njia ya kuzungumza na vyombo vya Habari ili waweze kwenda vituoni kwa watendaji wa kata kuchukua vitambulisho vyao ambavyo tayari vipo tayari.

Kwa upande wake Afisa Usajili Grace Msacky, akizungumzia changamoto inayowakabili katika ofisi hiyo, alisema wanachangamoto ya wananchi kujiandikisha mara mbili mpaka tatu, hivyo wanapofika ofisini hapo wanataka kujiandikisha upya huku mfumo ukionyesha tayari ameandikisha, na pia baadhi ya wananchi ambao vitambulisho vyao zipo tayari hawaendio kuchukua lakini wanakuja kuomba namba ofisi ya mkoa na ulazimika kuwanyima ili waweze kwenda kwa watendaji wao wa Kata.

“Tuna changamoto moja ya wananchi wetu kujiandikisha mara mbili mara tatu, unakuta pengine ametumia taarifa tofauti hibvguo atrakapokuja hapa tukimwambia hutapata namba kwasababu umejiandikisha pengine huwa hawaelewi, pia kuna vitambulisho vimetoka vipo kwa watendaji, lakini haeataki kwenda kuchukua vitambulisho vyao na wanataka namba wakati tayari vitambulisho vipo, mheshimiwa naibu waziri tunaomba mtusaidie hilo,” alisema Grace.

Pia Naibu Waziri Chilo aliwataka watumishi hao kuwa na lugha nzuri kwa wananchi pamoja na kuwapa kipaumbele wasiojiweza ili waweze kupata msaada kwa kuwapa maneno mazuri na kuwahudumia wananchi hao ili waridhike kwa huduma zitolewazo na NIDA.

“Kwasababu mnatoa huduma na mnaowahudumia ni wananchi, ni binadamu, tumieni maneno mazuri, moja ya miongoni ya kazi kubwa tuliopewa na Mheshimiwa Rais Samia ni kuwahudumia wananchi, kwa mujibu wa shida zao na kwa mujibu ya taratibu zilizopangwa, hiyo ndio kazi kubwa, na nyie kazi yenu ni kuhudumia wananchi, tumieni lugha laini kuwatumikia,” alisema Chilo.

Chilo aliwataka watumishi hao licha ya uchache wa watumishi katika ofisi hiyo ya Mkoa, waendeleze umoja na ushirikiano kwa kufanya kazi zaidi na kazi zisikwame, kazi ziendelee kwa kuwatumikia wananchi kwa weledi.

Kwa upande wake, Msajili wa NIDA Mkoa wa Dodoma, Khalid Mrisho, alisema changamoto kubwa wanayoipata ofisi hiyo ni pale kazi zinapotangazwa nchini, idadi kubwa ya wananchi ufika katika ofisi hiyo kuomba namba, idadi inakuwa kubwa na watumishi ni wachache, hivyo ametoa wito wananchi kuja kuomba namba hata kama kazi hazijatangazwa.

No comments:

Post a Comment

Pages