HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 08, 2021

WANAKIJIJI MULEBA WATAKIWA KUPISHA ENEO LA MRADI

Wakazi wa kitongoji cha Rwenzige, kijiji Kiteme, kata ya Kasharunga wilaya ya Muleba wanaoishi kwenye eneo la mradi wa Ranchi ya Taifa ya mifugo (MWISA II) ambao mazao yao pia yapo kwenye eneo hilo wameelekezwa kuwa pindi wakimaliza kuvuna mazao yao awamu hii wahamie kwenye maeneo yao waliyotengewa ili kupisha eneo hilo la ranchi ya mifugo.

Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila alipoenda kutatua changamoto ambapo wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakigoma kuhama kutoka katika eneo hilo kwa kueleza kuwa wamewekeza mazao.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji hicho, Mhe. Toba Nguvila amewaambia wakazi hao kuwa kwa wale wenye mifugo watapata vitalu vya kufugia na kuwasisitiza kuunda ushirika ili waweze kujumuisha ng'ombe zao kwa pamoja kuweza kufikisha idadi ya ng'ombe wanaotakiwa kuwa kwenye kitalu.

"Wale wenye mifugo, kama una mifugo mingi kuanzia ng'ombe hamsini ukichukua kitalu huwezi kukimudu ila mkijiunga katika kikundi mkawa na ng'ombe hata 500 kwa pamoja kwa kuunda ushirika mnakodi kitalu chenu na tumesema kipaumbele cha kwanza cha kugawa vitalu hivi ni kwa wakazi wa eneo husika" ameeleza", Mhe. Nguvila.

Wakitoa malalamiko yao baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kero yao ni kuhamishwa kwenye mashamba ambayo tayari wameshapanda migomba na kahawa pamoja na pia kuongezewa maeneo ya kulima kwani wanayogawiwa ni maeneo madogo. Na kero hizi zimetolewa ufafanuzi kama ifuatavyo;

Akizungumzia juu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule Mhe.  Nguvila amewashauri wataalam wanaohusika na upimaji wa maeneo kwa wananchi kuongeza ukubwa wa eneo la shule kwani ekari 18 hazitatosha kujengwa shule.

Aidha, amewasisitiza wale wanaokaa maeneo ya mbali zaidi na makao makuu ya kijiji ni lazima warudi kwenye kitongoji mama ili kuweza kupata huduma za msingi kama elimu na afya pamoja na kuwa karibu na barabara ili hata pia waweze kuwa salama na mali zao.

Kuhusu kaya zenye familia kubwa kuanzia watu 10 na kuendelea amewaambia wakazi hao kuwa familia hizo kwa kila mmoja atatengewa eneo la ekari sita na kuwasisitizia kuwa wakishapewa maeneo yale hawatafukuzwa tena. Watabakia kwenye maeneo hayo waliyotengewa ili kupisha eneo kwa ajili ya vitalu na kuwa na makazi ya kudumu kwenye maeneo waliyotengewa.

Pia amewaeleza wananchi kuhusiana na suala la kuongezewa maeneo hawezi kulisemea moja kwa moja atajiridhisha mwishoni wakishagawiwa maeneo ya ekari sita kila moja na kuangalia uhalisia uko wapi ili kama kuna ulazima wataalamu watakaa na kuona namna ambavyo jambo hili litawekwa sawa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba Ndg. Greyson Mwengu amewasomea wananchi hao baadhi ya maazmio ya kikao kilichofanyika mwezi Julai 2021 na kuongozwa na Mwenyekiti wa kikao Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi akiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel, Mkuu wa wilaya, Wabunge wa majimbo ya Muleba Kaskazini na Muleba Kusini na Madiwani ambao maeneo yao yapo ndani ya mradi huo kuwa walikubaliana kwamba:

Katika eneo la Ranchi ya NARCO kwenye mradi huu asilimia 30 itakuwa kwa ajili ya ukodishaji kwa wafugaji wadogo ambao wapo eneo la Muleba na kwamba endapo wafugaji wadogo watahitaji eneo zaidi ya asilimia 30 hawazuiwi kukodisha maeneo kwenye eneo la asilimia 70 ya eneo la mradi wa NARCO na kwamba wataratibu utekelezaji kwa kusaidiana na Halmashauri ya wilaya ya Muleba.

Na katika makubaliano hayo pia walikubalina kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia tena eneo ambalo sasa limebainishwa kwa ajili ya mradi wa MWISA II na ifahamike kuwa uwepo wa maeneo ya ranchi yana manufaa kwa Taifa kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Mkuu wa wilaya ya Muleba Toba Nguvila akizungumza katika mkutano huo na wananchi.
Sehemu ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment

Pages