Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mataka akizungumza na wazazi wa kata ya Zuzu kwa lengo la kuboresha elimu katika kata hiyo.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapaleka watoto wao shule mpaka ifikapo Jumatatu ya wiki ijayo wakamatwe na kupewa kazi ya kufanya usafi shuleni na katika miradi ya Serikali ambayo inaendelea kujengwa Mkoani hapa.
Pia amewaagiza watendaji wa Mitaa mitano katika Kata ya Zuzu Jijini Dodoma kuwatafuta na kuwakamata wazazi na walezi wa watoto 88 ambao hawajaripoti masomo ya kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Zuzu tangu shule zifunguliwe Januari 17 mwaka huu.
Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Zuzu kwa lengo la kuboresha ufaulu shuleni hapo ambapo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana 2021 ilishika nafasi ya 51 kati ya shule 52.
Amesema kuwa wazazi na walezi hao wangeona umuhimu wa kuwa na kipaumbele katika elimu kwa kuhakikisha waatoto wao wanahudhuria masomo na kufuatilia mienendo yao.
"Jumatatu ya wiki ijayo nitafanya msako wa nyumba kwa nyumba kujua ambao watakuwa wamekaidi agizo hili,nawaambia Magereza huwa haijai,"amesema.
"Watendaji wa mitaa ya Mazengo Pinda,Sokoine,Soweto na Chididimo katika Kata ya Zuzu hakikisheni wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanafika shuleni haraka iwezekanavyo ili kuanza masomo mara moja,"amesisitiza
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa wale wote ambao watakuwa wamekaidi agizo hili migambo itatumika kuwakamata ikiwa ni pamoja na kuwapa jukumu la kufanya usafi katika vyoo vya shule pamoja na katika miradi ya Serikali.
Ameongeza kuwa mzazi ambaye mwanae atakuwa hajaripoti shuleni akamatwe akasafishe vyoo huku watoto wakiwa wanaona ikiwezekana wawe vibarua katika miradi inayoendelea kujengwa na Serikali.
"Mzazi atakaye mpeleka mtoto wake shule binafisi (Private ),simu ipigwe shuleni waulizwe. Kwa hili sitaanii nitalisimamia kwa nguvu zangu zote na watakaofanya hivyo atahakikisha anakimbia nyumba yake," ameongeza.
“Sitaki kusikia mtoto anabaki nyumbani anataka aje shule,kwangu mtaelewa kwanguvu na hapa ninamanisha sina utani katika hili hatuwezi kujenga nitahakikisha mpaka mnakimbia nyumba zenu sitaki utani katika hili,”amesema Mataka.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza atafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwatafuta wale wote ambao watakuwa wamekaidi agizo hilo huku akitaka kila mzazi kubeba jukumu lake.
Amewataka wazazi kuwasaidia wanafunzi waweze kutimiza ndoto zao za kusoma na kuacha kulalamika kwamba wanatembea umbali mrefu.
“Kila mzazi abebe hasira za kuhakikisha mwanae anasoma na kufaulu agenda ya elimu iwe kipaumbele kwa kila mmoja sitaki kusikia habari ya maneno maneno wanafunzi wanatakiwa kusoma,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo ,Dismas Chilala amesema wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa wazazi na wanafunzi kuhusu umuhimu wa elimu na kwamba wengi wamekuwa hawamalizi shule kutokana na sababu mbalimbali.
“Kuna changamoto Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mtazamo wa wazazi hawaelewi umuhimu wa elimu ni nini katika jamii na manufaa yake ni yapi,hapa wengi wanaoanza kusoma hawamalizi,”amesema
Kwa upande wake,Diwani Kata ya Zuzu,Awadh Abdallah amebainisha kuwa changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuchukuliwa na kwenda kufanya kazi za ndani pamoja na wengine kutokuripoti shuleni.
Amesema kunahitajika jitihada kuhakikisha wanafunzi wanaoonza kidato cha kwanza kuwasaidia mpaka wamalize kidato cha nne kwani wengi wamekuwa hawamalizi.
Diwani huyo amefafanua kuwa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa kilomita 6 kutoka Chididimo hadi Zuzu aliutatua kwa kutoa nyumba ili wanafunzi waweze kukaa na kutakiwa watoe shilingi 15,000 kugharamia maji na chakula lakini wengi walikataa.
No comments:
Post a Comment