HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 24, 2022

Dunia yataka taarifa za hali ya hewa kupewa kipaumbele


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 23, 2022 wakati wa maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani. 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi.

 

Na Irene Mark

MIAKA 69 baada ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), watanzania wamesisitizwa kuzipa kipaumbele taarifa za hali ya hewa ili kupunguza athari za majanga yatokanayo na hali ya hewa.

Akizungumza Dar es Salaam leo Machi 23, 2022 wakati wa maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa amekiri kuongezeka kwa majanga ya hali ya hawe hivyo lazima tahadhari za mapema zitolewe na hatua zichukuliwe.

Waziri Mbarawa amewasisitiza wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kuimarisha mipango yao katika kufanya shughuli za kila siku za maendeleo.

Akinukuu kaulimbiu ya siku ya hali ya hewa duniani isemayo ‘Tahadhari kwa Hatua za Mapema’ Waziri Mbarawa alisema ni muhimu kufuatilia taarifa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ili kuchukua tahadhari mapema kukabiliana na majanga.

“Serikali yetu inaendelea kuwekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya kisasa kwaajili ya mamlaka hii lakini kubwa zaidi tunawekeza kwenye rasilimali watu wenye utaalam wa kutosha kutumia vifaa hivyo ili kupata taarifa bora zaidi zenye usahihi.

“...Hivi sasa usahihi wa taarifa za TMA kuhusu utabiri na hali ya hewa kwa ujuma umeongezeka tupo kati ya asilimia 93 hadi asilimia 96 hiki ni kiwango kizuri sana lakini tunatamani kupata usahihi ikibidi hata asilimia 99.5 ndio maana tunaendelea kuwekeza kwenye ununuzi wa rada na wataalam huku tukizingatia makubaliano ya mkataba wa Minamata unaozitaka nchi zote kuachana na matumizi ya vifaa vinavyotumia zebaki,” alibainisha waziri huyo.

Akihitimisha maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani, Waziri Mbarawa alisema hakuna maendeleo bila hali ya hewa hivyo ni vema taarifa za TMA zikawafikia watanzania wote kwa wakati nao wakazitumia kupanga shughuli zao za kila siku ambazo ndio msingi wa maendeeo yao na taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alisema kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuieleza dunia kwamba majanga ya hali ya hewa yameongezeka kwa idadi na ukubwa wake.

“Mathalani vimbunga kwa miaka ya hivi karibuni vimeongezeka, msimu moja unaweza kuwa na vimbunga viwili hadi vitatu kwa hiyi athari zinakuwa kubwa hivyo watu wakichukua hatua mapema haya majanga yatapungua,” alisema Dk. Kijazi na kuongeza ndio maana mamlaka yake inatoa tahadhari mapema ili wananchi wachukue hatua za mapema pia.

No comments:

Post a Comment

Pages