Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Nchini Bw. Zlatan Milisic, wakibadilishana hati za makubalino za mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia tarehe 1 Julai 2022 hadi 30 Juni 2027, baada ya kusainiwa jijini Dodoma.
Na Eva Valerian, WFM - Dodoma
Taasisi ya Umoja wa Mataifa imeipatia Tanzania msaada wa jumla ya dola za Marekani bilioni 1.85 ambazo ni takribani shilingi trilioni 4.3, kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali katika maeneo waliyokubaliana yakiwemo sekta ya maji, afya, elimu, kilimo na jinsia na usawa kati ya shughuli za wanawake na wanaume.
Makubaliano ya Msaada huu yametiwa Saini Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Tanzania Bara na Visiwani, na Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa Bw. Zlatan Milisic kwa niaba ya shirika hilo.
Bw. Tutuba alisema kuwa kiwango hicho cha fedha kimeainishwa kwenye shughuli mbalimbali lakini kitakuwa ni kiwango cha kuanzia na baadae inawezekana wakati tunaendelea kutekeleza programu mbalimbali, kama patajitokeza wadau watakaoongeza miadi yao, viwango vitakuwa vina badilika na vitaingizwa kwenye bajeti ya kila mwaka ya Wizara au Halmashauri na Mikoa husika.
“Utaratibu mpya ambao ni endelevu wa ushirikiano kati ya Taasisi za Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeona msaada huu wa fedha utaweza kutekeleza afua mbalimbali katika maeneo tuliyokubaliana, na kwa kuwa tumefanya majadiliano katika kuandaa programu hii ya miaka mitano, tutaanza kutekeleza tarehe 01 Julai 2022 mpaka tarehe 30 June 2027” Alisema Tutuba.
Aidha Bw. Tutuba alisema katika programu hii maeneo yatakayoguswa yatachangia katika ukuaji wa uchumi, yatapunguza umasikini na kuboresha huduma mbalimbali za ustawi wa jamii. Shughuli nyingine ambazo zinaendana na vipaumbele vya Taifa vya miaka mitano kwa upande wa mpango wa tatu wa miaka mitano ya Tanzania Bara na Visiwani, kulingana na maeneo yaliyobainishwa kwenye dira ya maendeleo ya Zanzibar.
Kwa Upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa Bw. Zlatan Milisic, alisema kuwa walifanya utafiti kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu na kubaini maeneo watakayoyapa kipaumbele na kutoa msaada kwa Tanzania Bara na Visiwani. Hivyo wameiomba Serikali ya Tanzania kufanya utaratibu wa kuzindua programu hii mpya ya miaka mitano ya ushirikiano.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Kamati ya usimamizi wa ushirikiano kati ya Serikali na mashirika ya umoja wa mataifa nchini Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wakiwemo watendaji wa Serikali.
No comments:
Post a Comment