Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SHIRIKA
la Marie Stopes Tanzania (MST) kwa kushirikiana na Flaviana Matata
Foundation, wameadhimisha siku ya hedhi salama kwa kutoa elimu kwa
wanafunzi 987 wa kike na kiume wa Shule ya Sekondari ya Bukandwe,
wilayani Magu Mkoa wa Mwaza.
Siku ya hedhi duniani huadhimishwa
kila mwaka Mei 28 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu maswala ya hedhi
kwa msichana na kuhamaisha upatikanaji na matumizi ya maji safi na taulo
za kike hasa walio katika mazingira magumu.
Taarifa kwa vyombo
vya habari iliyotolewa na Meneja Mawasiliano wa MST, Esther Shedafa
imeeleza kwamba dhumuni la maadhimisho ya siku ya hedhi ni kumtaka binti
ajisitiri vizuri akiwa kwenye siku zake huku akiendelea na masomo yake
na shughuli nyingine.
Shedafa amesema wanafunzi wakiume wameshiriki kwenye siku hiyo ili kuondoa unyanyapaa pale msichana anapokuwa kwenye hedhi.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo siku ya hedhi mwaka huu imebebwa na kauli mbiu
isemayo ‘Hedhi iwe kama ni moja ya Maisha ya kawaida kwa msichana na
mwanamke’.
“Hii kaulimbiu ina maana kwamba tuwe na Dunia ambayo
hakuna mtu ataachwa nyuma au atashindwa kufikia malengo yake au kufanya
shughuli zake za kila siku kwa sababu tu anaingia kwenye siku za hedhi,”
ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo kutoka kwa Shedafa.
Hata hivyo
MST na Flaviana Matata Foundation wametoa wito kwa mashirika binafsi,
walimu na serikali kusisitiza utolewaji wa elimu ya hedhi kwa vijana wa
kiume na wa kike ili kuwasaidia wasichana kutambua mabadiliko ya mwili
na kukabiliana nayo ikiwemo namna bora ya kujisitiri na kuondoa
unyanyapaa pale msichana anapokuwa kwenye hedhi .
“Hedhi ni
kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa, wakati
ambao kwa kawaida unarudi kila mwezi ambapo hutokwa na damu kwenye uke
kwa sababu kijiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko cha vijiyai
kisipopata mbegu ya mwanamume baada ya siku moja kinaharibika
harakaharaka.
“...Na hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi,
iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inajiengua na kutoa
damu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Shedafa.
Ilieleza
kwamba hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike kupata
mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi ambayo ni
taulo za kike maji safi na salama na sehemu ya kubadilishia.
Wataalamu
wa afya wanasema kuwa mtoto wa kike akipata hedhi salama basi
ataondokana na matatizo ya kiafya ikiwemo miwasho, fangasi, maumivu na
hedhi bila kutokwa damu nyingi, hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.
“Suala
la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike. Hata hivyo, imekuwa
tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao hupata wasiwasi na kukosa raha
pindi wanapokaribia mzunguko wao.”
MST imewataka wananchi kuwasiliana nao kwa namba ya simu 0800753333 bila malipo katika vituo vyao
vilivyopo Dar es salaam, Zanzibar, Mwanza, Musoma, Kahama, Arusha , Iringa , Makambako na Kimara.
Hata
hivyo baada ya mafunzo mashirika hayo yaliwashika mkono wanafunzi hao
kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo taulo za kike kwa wasichana.
No comments:
Post a Comment