HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 18, 2022

‘HEET’ YAANZA KWA KUWAJENGEA UWEZO WANATAALUMA WA MZUMBE

Mwezeshaji wa mafunzo, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi, Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Jenipher Sesabo, akitoa mafunzo  kwa washiriki. 

Dkt.Nicholous Tutuba, Mnufaika wa mafunzo akichangia mada wakati wa mafunzo.



Wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe wameanza kupatiwa mafunzo ya kuboresha na kuandaa mitaala mipya kupitia mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu Kiuchumi ‘HEET’ ulioanza kutekelezwa na chuo hicho hivi karibuni, baada ya fedha za mradi kutolewa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akizungumza katika warsha iliyofanyika Kampasi Kuu Morogoro, Mratibu wa mafunzo ya mitaala kupitia mradi wa ‘HEET’ Dkt. Joseph Sungau, amesema warsha hiyo imelenga kuwawezesha wanataaluma kuhuisha na kuandaa mitaala mipya kwa kuzingatia miongozo iliyopitishwa itakayowezesha kuandakiwa Program mpya zinazoendana na soko la ajira pamoja na kuongeza udahili wa Wanafunzi, ambalo ndiyo lengo kuu la mradi wa “HEET”.

“Tunategemea ndani ya miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huu, mitaala 15 ya Chuo Kikuu Mzumbe itakuwa imeboreshwa na mipya kuanzishwa, na katika miaka mitano ya mradi tutakuwa tumepata wahitimu watakaokuwa wanakidhi mahitaji ya soko la ajira, kutokana na mitaala mipya iliyoboreshwa” alisisitiza Dkt.Sungau.

Katika hatua nyingine Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt.Jenipher Sesabo, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatapelekea mabadiliko chanya ya kiuchumi, hususani katika kipindi hiki ambacho Taifa limejielekeza katika kuimarisha uzalishaji wa viwanda. Amesisitiza wahitimu wanatakiwa kuwa na ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine, badala ya dhana ya sasa iliyojengeka miongoni mwa wengi ya kuajiriwa

Kwa upande wao wanufaika wa mafunzo hayo wamesema yatawasaidia kutengeneza mitaala inayohitajika sokoni kwani wengi wao hawakuwa na uelewa kuhusu mchakato mzima wa kufanya maboresho ya mitaala na kuanzisha mitaala mipya, ikiwemo kufanya uchambuzi yakinifu wa mahitaji ya soko pamoja na kujifanyia tathmini binafsi.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwani leo tumeweza kujua umuhimu wa kufanya tathimini ili kutambua ikiwa tunachowalisha wanafunzi wetu ndicho kinachohitajika sokoni.  Ni vema wanataaluma wengi zaidi wakapata mafunzo haya yatakayowawezesha kutengeneza program zinazokidhi mahita ya soko”. Alisema Dkt. Nicholous Tutuba Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe.

 

MAELEZO YA PICHA:

1.     

 

2.     Baadhi ya Washiriki wa mafunzo wakimsikiliza kwa makini  mwezeshaji wa mafunzo (hayupo pichani).

 

3.     Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Anosisye Kesale, akichangia mjadala wa uboreshaji mitaala wakati wa mafunzo.

 

4.     Dkt.Nicholous Tutuba, Mnufaika wa mafunzo akichangia mada wakati wa mafunzo.

 

5.     Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Patrick Kihoza, akichangia mada wakati wa mafunzo.

 

6.     Washiriki wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mada wakati wa mafunzo.

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages