Na John Richard Marwa
Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 23 (U 23) Leo inashuka Dimbani kuwavaa Nigeria Mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afcon, katika Dimba la Benjamin Mkapa.
Kikosi hicho cha U23 kitashuka ugani majira ya saa 10 jioni kumenyana na Nigeria ikiwa ni harakati za kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Afcon U23.
Akizungumza kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Timu hiyo Hemmed Morocco amesema kikosi chake kiko tayari kuwavaa Nigeria na anaamini wataibuka na ushindi licha ya kuwa utakuwa mchezo mgumu.
"Kikosi chetu kiko tayari na Maandalizi yamekamilika kuelekea mchezo huu, tunafahamu umuhimu wa mchezo huu na ugumu wake lakini mchezo tofauti na iliyopita.
"Wachezaji wako tayari na sisi benchi la ufundi tumeshanaliza maandalizi yote ambayo yatatuwezesha kuibuka na ushindi. Nigeria ni timu ngumu lakini haiondoi dhamira yetu ya kupata matokeo tukiwa nyumbani."
Morocco amesema kikosi chake kitawakosa nyota watatu ambapo Kelvin John na Novatus Dismas hawajajiunga na timu na Abdul Sopu ambaye ni majeruhi.
"Nyota wetu Novatus Dismas na Kelvin John hawajaruhusiwa na klabu zao kutokana na mchezo huu kutokuwa kwenye kalenda ya FIFA. Tunajitajidi kama itawezekana tuweze kuwapata kwenye mchezo wa marejeano.
"Lakini pia tunamkosa Abdul Suleiman Sopu ambaye ni majeruhi. Kukosekana kwa wachezaji hao hakujapunguza kitu kwa sababu tuna kikosi cha wachezaji wengi na ambao wako tayari kwa mchezo huu." Amesema Morocco
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Ally Msengi amesema wao kama wachezaji wanafahamu wanaenda kucheza na timu nzuri hivyo watanzania wajitokeze kuwapa sapoti katika mchezo huo.
"Kama wachezaji tuko tayari, tunafahamu tunaenda kucheza na timu nzuri na ngumu hivyo tuko tayari kukabiliana na huo ugumu. Kikubwa watanzania wajitokeze waje kutusapoti sisi tunawaahidi ushindi." Ally Msengi.



No comments:
Post a Comment