Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu ametakiwa aache uzushi na siasa za uongo kuhusiana na bei ya zao la karafuu na madai kuwa ni kampuni moja pekee ndio imepewa zabuni ya ununuzi.
Akizungumza leo 19 Septemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema pia ni jambo la hovyo kuzusha na kumsingizia marehemu Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa eti ndiye aliyepandisha bei ya karafuu jambo ambalo si kweli kwani hakuwa na mamlaka hayo.
Mbeto alisema hivi sasa bei ya karafuu imefikia Tsh.31,000 kwa kilo na amemtaka Makamu Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo, apunguze uzushi na uongo kwani mambo hayo yanakipunguzia chama uaminifu kwa wananchi kama kweli kinataka kuwa chama makini cha siasa na kumuasa asifanye komedi kwenye mambo ya msingi yanayohusu maisha ya watu.
Mwenezi Mbeto alisema Jussa akiwa katika mkutano wa kampeni Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja alidai kuna urasimu na ni kampuni moja ndio imehodhi ununuzi wa Karafuu za Zanzibar jambo ambalo si kweli.
Pia Jussa anadaiwa kuwaongopea watu wa Fuioni kuwa eti, Marehemu Seif Sharrif Hamad ndiye aliyepandisha bei ya karafuu wakati si kweli kwa maana hakuwa na mamlaka hayo.
Mbeto alibainisha, zabuni hutangazwa na serikali na Kampuni zenye uwezo hupewa kazi hiyo ya kununua karafuu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Mbeto ameyataja makampuni yanayonunua karafuu Zanzibar kupitia ZSTC ni pamoja na Unit Trader ya India, Afcom Trading ya Dudai, Brookes Ltd, KK Global, Zenj Spice, RKK ya India na Rho Traders African ya nchini Afrika Kusini.
“Makampuni ya nchi tofauti yananunua karafuu Zanzibar na si kama anavyozusha kuwa ni mtu mmoja ndio anayeinunua” alisema Mbeto.
Alisema mwenezi huyo kuwa mwanasiasa huyo na wenzake wa ACT Wazalendo, hawajui athari za uongo kwenye siasa na faida za ukweli na uwazi katika dhana nzima ya siasa safi na uongozi bora.
“Kabla na baada ya mapinduzi serikali iliwakodishia mashamba ya karafuu wananchi hivyo hawakuwa na umiliki nayo lakini Dkt, Mwinyi kawamilikisha” alisema na kuongeza na hivi karibuni watakabidhiwa hatimiliki zao.



No comments:
Post a Comment