HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 07, 2025

Mbeto 'amvaa OMO' kuhusu kura ya mapema Zanzibar

Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha  Mapinduzi  kimesema kwa mujibu wa Sheria  hakuna chama  chochote  cha Siasa, Vyombo vya habari au Taasisi  yoyote  yenye Mamlaka ya kutangaza matokeo ya Uchaguzi bila idhini ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)


Pia chama hicho kimesisitiza kuwa  Uchaguzi  katika nchi  yoyote duniani  ,  huongozwa kwa kanuni na  taratibu  za kisheria  si  kwa mtindo holela .

Msimamo huo   umetolewa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar,  Idara  ya Itikadi ,Uenezi na Mafunzo,  Khamisi  Mmbeto Khamis,  wakati  akijibu hoja zilizotolewa na mgombea urais wa ACT  Wazalendo ,Othman Masoud Othman  .

Othman mara baada ya kuchukua  fomu  ya kuwania Urais, amesikika akiikosoa Sheria ya Kura ya mapema akitishia na kutaka isitumike . 

Mbeto  akijibu hoja hiyo alisema, sheria hiyo haikutungwa aidha na malaika, majini au mashetani, bali  imetungwa na binadamu  waliopewa dhamana ya  kutunga na kuzipitisha.

Alisema sheria  hiyo itaendelea  kutumika Zanzibar hadi pale  Baraza la Wawakilishi Zanzibar, litakapofanya mabadiliko mengine kwa utaratibu  halali. 

"Hakuna Sheria nzuri au mbaya ikiwa imeshatungwa pia  imepitishwa na  Baraza la  Wawakilishi Zanzibar. Sheria  ya kura ya mapema imeridhiwa na chombo  hicho . Haikutungwa katika ofisi ya chama chochote  cha siasa" alisema Mbeto.

Katibu mwenezi huyo, alisema ni wazi ACT kupitia  mgombea wake  wa Urais , kimebaini kushindwa kwa kuona maendeleo  yalivyoshamiri huku wananchi wakisifu uongoozi wa Rais Dk  Hussein Ali  Mwinyi.

"Hayupo  mwenye ubavu  wa kuzuia watu wasipige kura ikiwa sheria inataka hivyo. Atakaewatisha, kuwazuia au kutaka kuwapiga wapiga kura wasifike vituoni watadhibitiwa  na mkono wa sheria " alisema Mbeto. 


Pia katibu  huyo  Mwenezi  aliongeza kusema kuwa ikiwa  Othman ameshajua kuwa hawezi kushinda si kosa kwake  kutangaza kuwa amekubali kushindwa.

"Sheria  anayoipinga  imetungwa na wajumbe halali wa Baraza la Waawakilishi Zanzibar. Inawezaje kufutwa leo  ikiwa chombo hicho kimevunjwa kisheria ?" Alihoji  Mbeto.

Mwenezi  huyo alisema anachokitaka Othman kuwashawishi vijana wa ACT ili walete ghasia na fujo kwa kisingizio  cha sheria ya kura za mapema ambayo imekuwa ikitumika katika Mataifa mengi  duniani.


 

No comments:

Post a Comment

Pages