Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaenda kwenye kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba 2025 kuwakumbusha wananchi ahadi walizotoa walipoenda kuomba kura miaka mitano iliyopita na kuwaonyesha walichofanya.
Akizungumza Mjini Unguja, Katibu wa Kamati Maalum NEC, Taifa Khamis Mbeto Khamis alisema kama afanyavyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni zake ndicho anachoenda kufanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kampeni zake zitakazozinduliwa 13 Septemba 2025.
Mbeto alisema wanataka wawakum bushe ahadi walizotoa na kuwaonyesha jinsi zilivyotekelezwa kwa vitendo na Rais Dkt. Mwinyi na sio maneno matupu.
“Tunakwenda kuwakumbusha walichotaka tuwatimizie, tulivyoahidi na jinsi tulivyo tekeleza” alisema na kuongeza kuwa kuona ni kuamini.
Alibainisha kuwa Unguja na Pemba ahadi zimetimizwa na zingine kuvuka ilani ya CCM na kila sekta imeguswa na miradi inatekelezwa na mingine imekamilika.
“Tulio waahidi hospitali tutaenda kuwaonyesha, maana hivi sasa kila wilaya ina hospitali zenye hadhi, madaktari wanaokidhi mahitaji, dawa na vifaa vya kutosha,
waliotaka barabara wanaziona Pemba na Unguja, maeneo ya uwekeza, bandari zinazojengwa ikiwemo ya Shumba Mjini bandari jumuishi Mangapwani.
Bandari hiyo ikikamilika itakuwa yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mafuta na mizigo ambazo hivi sasa zinatia nanga bandari ya Mombasa na meli ndogo zinapakua mizigo kupelekwa Dar es Salaam na Malindi, Zanzibar kwa meli ndogo.
Licha ya uwekezaji huo masoko mapya ya kisasa, viwanda katika maeneo ya uwekezaji, barabara za juu (Flyover), viwanja vya ndege na miradi mingine ya kijamii.
“Miradi ni mingi sana na yote waZanzibari na waTanzania kwa ujumla wanaiona kwa macho yao na sio kuambiwa” alisema mwenezi na kubainisha kuwa upinzani umeishiwa hoja.
Alisema ndio maana mwingine ana sera ya Ubwabwa, ataruhusu kilimo cha bangi ili waTanzania wote wawe na changamoto ya afya ya akili.



No comments:
Post a Comment