HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2025

Othman Masoud: Wazanzibari wapo tayari kwa Mabadiliko

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema muitikio mkubwa wa wananchi kwenye kampeni za chama hicho ni ishara kwamba Wazanzibari walio wengi wapo tayari kuandika historia mpya ya nchi yao.

Akihutubia maelfu ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kwenye uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Tibirinzi, Chake Chake Pemba, Othman alisema ameamua kugombea urais akiwa na dhamira ya dhati ya kutimiza kiu kubwa ya Wazanzibari ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa miaka mingi.

Alisema zama za subira zisizo na kikomo, ambazo ziliwahi kuhubiriwa na Almarhum Maalim Seif, zimepita na sasa ni wakati wa kusimama imara kudai haki ya Zanzibar.

Aidha, akigusia Muungano uliopo baina ya Zanzibar na Tanganyika, Othman alisema ni aibu kubwa kuona Zanzibar ikiendelea kunyanyasika. Alisema hata muasisi wa Muungano huo, Hayati Abeid Amani Karume, alipinga baadhi ya dosari zilizokuwamo, lakini hadi leo hakuna hatua zilizochukuliwa kuzirekebisha.

"Zanzibar inahitaji Muungano wa usawa, unaotoa fursa sawa kwa pande zote mbili, na si huu uliopo sasa unaonufaisha zaidi upande wa Tanganyika. Hili linawezekana tu iwapo Wazanzibari watanipa kura zao Oktoba 29, ili tuanze safari mpya ya heshima na usawa," alisema.

Othman pia aliwashutumu CCM kwa kutumia macho kufumbia matatizo ya msingi ya Zanzibar na badala yake kuruhusu nchi izidi kudidimia, huku wachache pekee wakinufaika kwa maslahi yao binafsi.

Akibainisha hatua atakazochukua endapo atachaguliwa Rais wa Zanzibar, Othman alisema atahakikisha changamoto hizo zinamalizika mara moja kwa kuweka msingi imara wa demokrasia na haki.

Aliahidi kusimamia mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya ya Zanzibar, itakayohakikisha uhuru wa kila mtu, tume huru ya uchaguzi, vyombo vya haki vinavyofanya kazi kwa uwazi, na uwajibikaji wa viongozi wote bila upendeleo.

"Katiba mpya itatoa nafasi ya kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza na kuwachukulia hatua wahalifu wote, ili hakuna mtu atakayejiona yuko juu ya sheria. Hii ndiyo Zanzibar mpya tunayoiandaa," alisema kwa msisitizo.

Kwa mujibu wa Othman, Katiba hiyo mpya pia itafungua njia ya Zanzibar kuwa na tume huru ya uchaguzi yenye heshima, ambayo itahakikisha kura ya kila mwananchi inalindwa na kuhesabiwa ipasavyo. 





No comments:

Post a Comment

Pages