HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 28, 2025

Yanga kinara mkwanja wa Goli la Mama CAF

MCHAKAMCHAKA wa raundi ya kwanza ya michuano ya klabu Afrika (Ligi ya Mabingwa Afrika - CAF CL na Kombe la Shirikisho Afrika - CAF CC), umekamilika kwa timu tano kati ya sita za Tanzania kufuzu raundi ya 32 Bora, huku zikifunga jumla ya mabao 20, yenye thamani ya Sh. Mil. 95 za Goli la Mama.


‎Goli la Mama ni zawadi ya pesa taslimu inayotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo klabu ya Tanzania inaposhinda mechi ya kimataifa, inapewa kiasi cha Sh. Mil. 5 kwa kila bao na katika msimamo wa vinara wa kuzoa pesa ndefu katika hatua hiyo, Yanga inaongoza ikitwaa Sh. Mil. 25 kati ya hizo Mil. 95.

‎Kiasi hicho kinatokana na Yanga kuichapa Wiliete Benguela SC ya Angola mabao 3-0 ugenini na 2-0 nyumbani, huku Azam FC na KMKM ya Zanzibar ambazo zitaumana zenyewe raundi ijayo, zikivuna kiasi cha Sh. Mil. 20 kila moja, baada ya kufunga mabao mawili katika kila mchezo dhidi ya El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini na AS Ports ya Djibouti.

‎Katika mechi za mkondo wa kwanza, Azam FC iliichapa El Merreikh Bentiu kwa  mabao 2-0 na kurejea kichapo hicho wakati wa marejeano Azam Complex jijini Dar es Salaam, huku KMKM ikiirarua AS Ports kwa mabao 2-1 kwenye kila mchezo, kwenye dimba hilo lililopo Chamazi, wilayani Temeke.

‎Singida Black Stars inayoshiriki CAF CC, imevuna Sh. Mil. 15, huku ikiiondosha Rayon Sports ya Rwanda kwa ushindi wa ujumla wa mabao 3-1 (yaani bao 1-0 ugenini na 2-1 nyumbani).

‎Wekundu wa Msimbazi wameambulia Sh. Mil. 5 tu iliyotokana na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Gaborone United ya Botswana, kabla ya kuambulia sare ya bao 1-1 katika marudiano jijini Dar es Salaam, sare ambayo haikuipa bonasi ya pesa kutoka kwa Goli la Mama kwa kuwa haikushinda mechi.

‎Mlandege ya Zanzibar ambayo ilikuwa katika michuano ya CAF CL, awali ilipigwa bao 2-0 walipowafuata Ethiopian Insurance, huku wakishinda nyumbani kwa mabao 3-2 na kuambulia Sh. Mil. 15 za Goli la Mama, lakini ikiyaaga mashindano hayo na kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutupwa nje msimu huu.




 

No comments:

Post a Comment

Pages