HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

April 18, 2026

JIMBO LA ISMANI LAGOMBEWA KAMA NYUKI

NA DENIS MLOWE, IRINGA 


WIMBI la makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Isimani limezidi kushika kasi, baada ya idadi kubwa ya wagombea kurejesha fomu katika ofisi za CCM Iringa Vijijini.

Miongoni mwao ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa, Dk. Tumaini Msowoya, ambaye amerejesha fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Isimani katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, baada ya kukamilisha taratibu zote za uombaji. 
Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Dk. Msowoya aliishukuru CCM kwa nafasi ya kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia, akibainisha kuwa dhamira yake ni kuwatumikia wananchi wa Isimani kwa uadilifu na uwajibikaji. 

Aliahidi kusimamia maendeleo ya sekta za kilimo, biashara na ajira kwa vijana endapo atapata ridhaa ya chama na wananchi.
Naye Mwanasheria Egidy Mkolwe amerejesha fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo, akieleza kuwa uamuzi wake unachochewa na dhamira ya kuwarudishia wananchi wa Isimani kile walichowekeza kwake tangu utotoni. 

Akitumia taaluma yake ya sheria, amesema anaona ni wakati muafaka kusaidia kutatua changamoto zinazolikabili jimbo hilo, hasa tatizo kubwa la ukame linaloathiri shughuli za kilimo na ufugaji. Aidha, ameweka msisitizo kwenye umuhimu wa elimu kwa watoto ili kuinua ustawi wa familia na jamii.

Kwa upande wake, Comrade Lazaro Francis Ngwira, mkazi wa Kata ya Kisinga, ameeleza kuwa uamuzi wake wa kuwania ubunge unatokana na ufahamu mpana wa historia na changamoto za Jimbo la Ismani, ambako amelelewa na kuhitimu elimu ya msingi. 
Amedai kuwa uzoefu wake katika uongozi wa vyama, shughuli za utawala na utetezi wa haki za wananchi unampa uwezo wa kulitumikia jimbo hilo kwa ufanisi.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mtemaluge Mwilapwa naye amerudisha fomu ya kuwania ubunge, akieleza kuwa pamoja na kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini, moyo wake umekuwa ukimwita kurejea nyumbani Iringa Vijijini. 

Amesema uzoefu wake wa uongozi katika serikali na chama, pamoja na uelewa wa mahitaji ya wananchi wa vijijini na mijini, vimempa ujasiri wa kuomba nafasi hiyo ili kuendeleza kazi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge, marehemu William Vangimembe Lukuvi.

Claudio Francis Zwaga, ambaye pia amerejesha fomu, ameweka msisitizo kwenye maboresho ya huduma za afya, hususan bima ya afya kwa wananchi, pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama ili kumtua mama ndoo kichwani. Katika sekta za uzalishaji, ameahidi kuimarisha kilimo, ufugaji, uvuvi na masuala ya ardhi ili kupunguza migogoro. Zwaga, ambaye ni mfamasia na mkufunzi wa vyuo vya afya, amesema pia atatoa kipaumbele kwa michezo na sanaa kama njia za ajira kwa vijana.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika Jimbo la Isimani unaendelea kwa sheria na taratibu za CCM, huku wananchi wakifuatilia kwa ukaribu namna wagombea mbalimbali wanavyojipambanua kupitia sera na dhamira zao za kuleta maendeleo katika maeneo yote ya jimbo hilo.

Baadhi ya wagombea maarufu wanaosemekana wamejitokeza kugombea jimbo la Ismani ni mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Alfu Abri na aliyekuwa mpinzani wa Lukuvi Festo Kiswaga.




No comments:

Post a Comment

Pages