HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

April 22, 2026

Masauni: Mafanikio ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kutatuliwa kwa hoja za Muungano

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yussuf Masauni amesema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kutatuliwa kwa hoja za Muungano chini ya Ofisi hiyo.

 

Amesema hayo wakati akifafanua hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/27 aliyoiwasilisha bungeni jijini Dodoma Aprili 21, 2026.

 


Mhandisi Masauni alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia hoja 11 zimetatuliwa hadi kubakia hoja tatu ambazo hivi karibuni mbili kati yake zinatarajiwa kutatuliwa kupitia vikao vya Kamati ya pamoja ya Serikali zote mbili.

 

“Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tunakwenda kuifanya Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa ya kuzungumzia fursa na si hoja za Muungano,” alisisitiza.

 

Aidha, Mhandisi Masauni alisema kuwa Ofisi imekuja na mpango kabambe wa elimu kwa umma kuhusu Muungano ambao unalenga mambo mengi huku mojawapo linagusia mambo ya vijana.

 

Aliongeza kuwa amezingatia maoni ya wabunge kuhusu utoaji wa elimu ya Muungano ambapo alibainisha kupitia midahalo, mitandao ya kijamii elimu inatolewa na ndio maana zimetengwa fedha kwa ajili ya kuanzisha makavazi jijini Dodoma na Dar es Salaam ili kuhifadhi kumbukumbu za Muungano.

 

Katika kulipa nguvu ya kuwa mamlaka kamili Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Waziri Masauni alifafanua kuwa suala hilo lipo kwenye hatua nzuri na ni matarajio kuwa Bunge lijalo sheria itapelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa.

 

“Si kuifanya NEMC kuwa mamlaka kamili bali tunataka kuifanya NEMC kuwa ya kisasa zaidi, kupata vitendea kazi kama vile magari ya kutosha, mifumo ya kisasa kung’amua wapi kuna changamoto za kimazingira, tuwe na drones, boti za kisasa za kufika maeneo yote na tunataka katika kanda zote tuwe na vituo vya umahiri kama ilivyo kanda ya Geita,” alisema.

 

Kuhusu Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), alisema ni kweli bado fursa za biashara ya kaboni hazijatumika ipasavyo hivyo mkakati uliopo ni kuifanya biashara hiyo kuwa ni chanzo mojawapo cha mapato kwa kuingiza shilingi bilioni mbili kwa mwaka.

 

Awali akichangia hotuba hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Reuben Kwagilwa alisema kuwa Nguzo ya kwanza ya Dira 2025 inazungumzia uchumi imara jumuishi na shindani ambayo inazingatia uchumi unaokua kwa kasi unaobebwa na sekta binafsi.

 

Aidha, alieleza nguzo ya pili ni uwezo wa watu na maendeleo ya jamii ya kitanzania  inayoweza kuwa na afya, elimu bora na ujuzi kwa ajili ya kuendna na soko la ajira la dunia ya sasa.

 

Hivyo, alisema ili kuhakikisha yote haya yanafanyika nguzo ya tatu ni uendelevu wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ambayo imewekwa ili kusimamia rasilimali za taifa.

 

“Tumekaa na wataalamu tumekubalina tutumie dhamana hii ya kusimamia mazingira na taifa kwa ajili ya vizazi tunakwenda kuifanya kwa ufanisi, Mheshimiwa Rais ambaye ni kinara kwa mazingira Tanzani, Afrika na dunia amesaini kitabu hiki cha Dira anataka nguzo hizi zituelekeze kwenye uchumi wa dola trilioni moja kuhudumia watanzani ambao mwaka 2050 tutakuwa milioni 118 na pia anatakja tuwe na uchumi wa juu wa pato la kati.,” alisema Mhe. Kwagilwa.

 

Kwa hatua hiyo, Bunge la Jamhuri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais yenye jumla ya shilingi bilioni 99.9 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake katika mwaka wa fedha 2026/2027.


 

 

No comments:

Post a Comment

Pages