Na mwandishi wetu,
Sikonge
Kundi kubwa la Ng’ombe limevamia
eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA), Ipole wilayani Sikonge mkoani
Tabora ikiwa ni muendelezo wa wafugaji kukiuka sheria za uhifadhi.
Taarifa zilizotufikia jana, kutoka
kwenye eneo hilo la hifadhi zinasema, kundi la
Ng’ombe wanaokadiriwa kufikia 2000 lilionekana kwenye eneo hilo na mkuu wa wilaya ya Sikonge, Hadija
Mohammed, amesema mtu mmoja anashikiliwa na polisi kuhusiana na ng’ombe hao.
“Ni kweli matukio ya wafugaji
kuingia kwenye maeneo ya hifadhi hutokea na tunamshikilia mtu mmoja baada ya
kukutwa na Ng’ombe kwenye eneo hilo
jana (juzi).” Alisema DC huyo katika mahojiano ya simu jana.
Alisema, tatizo hilo wanajaribu kukabiliana nalo, na kupinga
taarifa kuwa wafugaji waliovamia kwenye hifadhi hiyo wanatoka maeneo ya nje ya
wilaya hiyo.
“Siyo kweli hakuna mfugaji yeyote
kutoka nje ya wilaya hii na huyu
tuliyemkamata ni msukuma wa hapa hapa, hakuna wamasai walioonekana kwenye eneo hilo labda taarifa hizo
mlizopewa siyo za kweli.” Alifafanua mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya
aliomba apatiwe muda zaidi ili afuatilie taarifa hizo polisi kwani hata jina la
huyo aliyemtaja kuwa amekamatwa alikuwa bado hajapatiwa.
Naye mwenyekiti wa hifadhi hiyo Nurdin
Kasanda alisema tukio hilo
lilitokea jana jioni (juzi), majira ya saa 12;45, ambapo askari wa eneo la
hifadhi waliokuwa doria walikamata ng’ombe wapatao 172.
Hata hivyo wakati wakijiandaa
kuchukua hatua za kisheria kwa kutoa taarifa polisi, kundi la wafugaji
lilivamia ofisi ya Hifadhi hiyo na kuwatorosha ng’ombe kwa nguvu.
Akielezea zaidi mkasa huo,
mwenyekiti huyo alisema, Desemba mwaka jana ng’ombe 400 walikamatwa kwenye eneo
la hifadhi, lakini wafugaji walijikusanya na kuwavamia askari na kuwanyang’anya
ng’omb hao.
“Kinachotusikitisha, taarifa za
uvamizi huu tuliziripoti polisi na tunaambiwa jalada la kesi yetu ndio kwanza
limepelekwa jana (Jumanne), huko Tabora kwa hatua zaidi za kisheria.”.
Alilalamika
Mwenyekiti huyo alimtaja kijana
aliyekamatwa kwenye vurugu za Jumanne, kuwa ni Luhende Ndege mwenye umri wa
miaka 17.





No comments:
Post a Comment