Na Bryceson Mathias, Mvomero
WANACHAMA wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Mvomero wamewaonya viongozi wa dini waliotia nia
ya kugombea uongozi katika chama chao wasithubutu kuwa mamluki, kwa kuwa watawashitaki kwa Mungu, na wakiendelea kwa shetani.
Akihojiwa na mwandishi kuhusu kuwepo
kwa tuhuma za viongozi hao wanaodaiwa kujipenyeza ndani ya Chadema
kama mamluki, Katibu wa Chadema Mvomero, Ramadhani Mrisho, amewaonya viongozi
hao kama wapo, kwa kuwa hakuna mharifu yeyote atakayepenya.
Hatua ya wanachama wa Chadema
Mvomero kuwaonya viongozi hao, imefuatia kuwepo kwa fununu za watia nia hao
kutumia fedha jimboni humo, ambapo walidai wanaunga mkono kauli ya Mwenyekiti
wao, Freeman mbowe, ambaye hivi karibuni akiwa Mbeya aliwaonya wagombea wa
Chadema kuwa asiwepo atakayethubutu kutumia
fedha kujipatia uongozi.
Mrisho alikiri kuwa anao viongozi
wa dini zaidi ya wanne kutoka madhehebu mbalimbali waliotia nia ya kugombea uongozi
tangu ngazi ya msingi hadi ubunge, huku akikiri na kusema kwa kutumia uwezo wao
wameweza kukifikisha chama hadi ngazi ya msingi.
“Hata mimi nimesikia minong’ono ya
nje ya chama kuhusu baadhi ya viongozi hao kudaiwa wanatumia nguvu ya fedha
kusaka uongozi huo. Lakini nataka nionye! Kama atatokea mwenye nia ovu
ya kukihujumu chama kwa njia hiyo, hatoki ng’o! Tutakula naye sahani moja!”
Aidha, alidai: “Nina imani kubwa na
Kamati Kuu ya Chadema Taifa, kwenye kura ya maoni na uteuzi wa wagombea, kwamba
itafanya kazi nzuri na ya haki, kutokana na
jinsi ilivyo makini, maana, taarifa zote inazo kabla ya jogoo hajawika. Hivyo
nina uhakika, kama mharifu yupo, hapenyi ng’o! Labda kamati iwe imeacha wajibu
wake,” alisema Mrisho.
Mapema katika mchakato wa kuwania ubunge
katika majimbo yanayoshikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yanayowindwa na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamejitokeza baadhi ya viongozi wa dini na
watia nia mamluki, wanaodaiwa kutumika kuudhoofisha umoja huo kwa nafasi hizo
ili kuwakwamisha Ukawa.
No comments:
Post a Comment