KAMATI ya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari
za Michezo nchini (TASWA) imeanza mchakato kuhusu marekebisho ya katiba ya
chama hicho kama ilivyoagizwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Kwa
mazingira hayo Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa zamani wa TASWA,
Boniface Wambura inaomba ushirikiano wa waandishi wote wa habari za michezo
nchini kufanikisha jukumu hilo kwa wakati uliopangwa na BMT, ili chama kifanye Uchaguzi Mkuu na kupata
viongozi wapya.
Kutokana na suala la muda kuwa
mfupi, Kamati imeandaa utaratibu wa kupokea maoni ya waandishi wa habari za
michezo kwa njia mbalimbali kabla ya kuiwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya
TASWA kupata baraka na kuitisha mkutano wa pamoja wa wadau kupitisha rasimu ya
katiba hiyo.
Wadau wenye maoni kuhusu mambo
wanayotaka yaongezwe au yapunguzwe katika Katiba ya sasa ya TASWA watume maoni
yao kwa email ifuatayo: katibataswatz@yahoo.com, katibataswa2018@yahoo.com na mwisho wa
kupokea maoni ni Jumanne Novemba 13, 2018.
Pia
wanaweza kufanya mawasiliano kwa ajili ya kupata nakala ya Katiba kwa Katibu
Msaidizi wa Kamati, Gift Macha kwa email machagift@gmail.com.
Kamati ya
Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa
TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka huu na badala yake BMT
ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona
namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.
Licha ya
Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi
wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari
Gift Macha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kamati.
Wajumbe ni
Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA,
Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.
Ahsanteni,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
07/11/2018
No comments:
Post a Comment