Mkurugenzi wa Bang! Magazine, Bi. Emelda Mwamanga akizungumza kwenye Kongamano la 'Woman of Influence, I'm Possible' jana kwenye Hotel ya Serena Dar es Salaam. Kongamano hilo pamoja na mambo mengine lilijadili namna wajasiriamali wanawake walivyo kabiliana na changa moto za janga la corona kwenye biashara zao.
Na Mwandishi Wetu
AKINAMAMA Wajasiriamali mbalimbali wamekutana
katika kongamano la 'Woman of Influence, I'm Possible' kujadili
changamoto za ugonjwa wa Covid 19 nchini kwenye shughuli zao na
kujadiliana namna ya kujikwamua na changamoto hizo. Kongamano hilo
lililoratibiwa na Mkurugenzi wa The East Africa Bang! Magazine, Bi.
Emelda Mwamanga limefanyika jana kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na wanawake wajasiliamali na wageni mbalimbali
ambapo mijadala na mada anuai ziliwasilishwa kuwajengea uwezo akinamama
hao.
Akizungumza na wanahabari katika kongamano hilo, Bi. Emelda
Mwamanga alisema lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha akinamama na
kujadili changamoto zilizojitokeza, kushirikishana namna ya kukabiliana
nazo na kuwajengea uwezo jamii hiyo kuweza kufanya vizuri zaidi kwenye
shughuli zao kwa mwaka ujao wa 2021. Alisema sehemu kubwa ya biashara
zikiwemo za kinamama ziliathirika kiasi kikubwa na ujio wa janga la
corona, hivyo kuna kila sababu ya kuyajengea uwezo makundi mbalimbali
wakiwemo akinamama wajasiriamali kuweza kukabiliana na janga hilo.
Alisema
Bang Magazine wamekuwa chachu ya kutamani maendeleo ya akinamama ndio
maana wamekuwa wakiwakutanisha kila mwaka tangu 2004, kusudi kubwa ikiwa
ni kumjengea uwezo mwanamke kwa kuwakutanisha na wenzao waliofanikiwa
zaidi ili waweze kuwasaidia wenzao kujikwamua zaidi kimafanikio.
Naye
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya ZARA Tours, Bi. Zainab Ansell
akizungumza kwenye Kongamano hilo, alisema wao kama wajasiriamali
wanawake waliopo katika sekta ya utalii wamejipanga kuhamasisha utalii
wa ndani ili kuziba pengo la upungufu wa watalii kutoka nje lililotokana
na janga la corona.
"...Sisi toka sekta ya utalii tumeanza
kuhamasisha utalii wa ndani kwa kuhamasisha jamii kuanza kutembelea
sehemu zetu mbalimbali za vivutio vya utalii, tayari tumefanya hivyo
hapo nyumba na sasa tunaandaa mapumziko ya mwezi Desemba, Siku Kuu ya
Krismas wengine waweze kutembelea mbuga zetu anuai na hata kupanda Mlima
wa Kilimanjaro," Bi. Zainab Ansell.
Alisema Tanzania ina sehemu
nzuri na za kujivunia za utalii hivyo Watanzania wanatakiwa kuelimishwa
na kuhamasishwa kuzitembelea; "Ukiangalia hata tozo za kutembelea mbuga
zetu kwa Watanzania zipo chini sana ukilinganisha na za wageni kutoka
nje ya nchi...kinachotakiwa ni kuelielimishwa na kuhamasishwa wao
kutembelea rasilimali hizo za taifa," alisema. Aliongeza kuwa kampuni ya
ZARA ina tozo maalum kwa Watanzania watakapenda kutembelea sehemu
mbalimbali za vivutio vya utalii ikiwa ni kuchochea utalii wa ndani kwa
jamii ya Watanzania.
Kwa upande wake, Mjasiliamali toka sekta ya
utalii, Bi. Leina Lemomo amesema wameanzisha ushawishi wa tozo maalum za
kiafrika (African rates) maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchochea
utalii wa ndani. Amesema ndoto zao ni kuona kunakuwa na tozo maalum kwa
Waafrika wanapotembelea nchi na maeneo mbalimbali ya bara la Afrika.
"Ndoto
yetu ni kuona kwamba kunakuwa na tozo maalum kwa ajili ya waafrika
tunapotembelea sehemu mbalimbali ndani ya Bara la Afrika, tunataka
ukisafiri kiutalii hata kwenye ndege kuwepo na punguzo la malipo maalum
kwa waafrika, vivyo hivyo kwenye hoteli mbalimbali barani Afrika...hii
inawezekana na inaweza pia kuchochea utalii wa ndani kwa Waafrika.
Ukienda mabara mengine tozo kama hizo zipo kwa raia wao na sisi hili
kuna haja ya kulipigia debe sote kwa pamoja," alisema Bi. Lemomo.
No comments:
Post a Comment