Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike akizungumza na viongozi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) jijini Dodoma mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Baraza hilo.
Na Jasmine Shamwepu, Dodoma
BARAZA
la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) limemuomba
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kukutana nao na kuzungumza kuhusu
mustakabali wa NGOs kwa maendeleo ya taifa.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) Lilian Joseph Badi
wakati wa kukamilisha zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Baraza hilo.
Lilian
alisema kuwa lengo la kutaka kukutana na Rais ni kuweka muelekeo mzuri
kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika jitihada za kuhakikisha
yanasaidiana na Serikali kuwaletea maendeleo wananchi katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali .
Lilian
aliongeza kuwa Baraza hilo litahakikisha linaleta umoja kati ya
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, wadau na Serikali ili kuhakikisha
inasaidia utekelezaji wa mipango mikakati iliyowekwa na Serikali katika
kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza
kwa niaba ya Serikali Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amelitaka Baraza hilo kufanya kazi
kwa kuzingatia Sheria taratibu na tamaduni za nchi ili kusaidiana na
Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika
kujiletea maendeleo.
Alisema
kuwa Baraza hilo linatakiwa kuhakikisha linaweka maslahi ya taifa mbele
na kuhakikisha linasimama badala ya Mashrika yote na sio kwa ajili ya
Mashirika machache tu.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt.
Richard Sambaiga amelipongeza Baraza hilo kwa kuchagua viongozi wake na
kuwataka kuwa jicho kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.
Hivi
karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima aliunda Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa
Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) ambao
umekamilika kwa kuchagua viongozi wa Baraza hili kuanzia ngazi ya
Wilaya hadi Taifa.
No comments:
Post a Comment