NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imezindua huduma mpya chini ya Mwamvuli wa Teleza Kidigitali
iitwayo NMB Onja Unogewe, ambayo imepongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Albert Chalamila, aliyeitaja kuwa ni zao la akili kubwa na ubunifu wa
wafanyakazi wa benki hiyo, unaoenda kuihakikishia jamii njia rahisi na salama
ya kupokea fedha na kufanya malipo.
Sambamba na hayo, RC Chalamila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi
uliofanyika Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, alisema NMB Onja
Unogewe ni huduma chanya iliyovuka mstari wa huduma za kibenki na kwamba
Serikali inaitarajia itaenda kuwa chachu ya kukuza elimu ya uhifadhi na
matumizi sahihi ya fedha kwa Watanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, RC Chalamila alisema Serikali inapongeza
ubunifu wa suluhishi za kifedha unaofanywa na NMB, huku akiitaja huduma hiyo
kuwa ni muarobaini wa upotevu wa pesa, uporaji, wizi, matumizi yasiyo ya lazima
na hatarishi nyinginezo zitokanazo na matumizi ya pesa taslimu.
"Mtaji mkubwa wa NMB tangu ilipoanzishwa (1997) hadi sasa inapokuwa kinara
wa huduma za kifedha nchini, ni watumishi wabunifu, walio na akili kubwa za
kufikiria suluhishi sahihi, rahisi, nafuu na salama za kifedha kama hizi. Kwa
miaka yote hiyo, benki 'imeji-transform' yenyewe na hiyo kuwa chachu ya kupaa
kwao kimafanikio.
"Kuna matarajio makubwa ya kufanya vizuri mara 20 ya ilivyo sasa katika
miaka kadhaa ijayo, kwa sababu NMB inaziona changamoto zitokanazo na matumizi
ya pesa taslimu kuwa ni fursa, ikaja na suluhishi hizi hizi za kidigitali
kusaidia jamii kuachana na utamaduni wa matumizi yasiyo sahihi na kuongeza
uhifadhi wa fedha zao," alisema RC Chalamila.
Aliwataka watoa huduma mbalimbali za kijamii wakiwemo waendesha bodaboda,
bajaji, mama lishe, wauza maduka, wafanyabiashara na wajasiriamali wa kada zote
jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya NMB Onja Unogewe
kwa kupata QR Code zao na kuzitumia kwa ustawi na ukuaji wao kiuchumi.
"Achaneni na utamaduni wa kutunza fedha kwenye vibubu majumbani ama kuweka
madukani, ambako hatari za upotevu, wizi ama ajali za matukio ya kuunguliwa
moto ni nyingi, kimbilieni katika suluhishi hizi matawini, chukueni QR Code
zenu na mfanye malipo kupitia hizo kwa usalama wa pesa za mtu mmoja mmoja na
kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa," alisisitiza.
Awali, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema
benki yake inajivunia sana bunifu za suluhishi za kifedha, alizozitaja kuwa ni
siri ya mafanikio ya benki hiyo, ambayo mwaka jana uliuongezea thamani Mwamvuli
wa Teleza Kidigitali ulioanzishwa mwaka 2019 kwa kuizindulia Huduma ya NMB Pesa
Wakala - huduma maalum ya kuweka na kutoa pesa kirahisi kupitia mawakala
wanaotumia simu za mkononi.
"NMB Onja Unogewe ni maboresho ya Huduma ya Lipa Mkononi 'QR Code,' ambayo
yanaenda kumpa wigo mpana mteja wa kulipia huduma kwa njia ya kidigitali,
ambako atanufaika na rejesho la asilimia 10 katika malipo yake.
Tunafanya hivyo kwa makusudi ili kuvutia zaidi watumiaji wa huduma zetu za
kimtandao ili kupunguza matumizi ya pesa taslimu.
"Pamoja na suluhishi hizi zote tunazobuni, kuzindua na kutoa kwa
Watanzania, bado tunao utamaduni endelevu wa kurejesha kwa jamii katika sekta
za elimu, afya na mazingira.
"Tayari tumepanda miti 500,000 kupitia Kampeni Endelevu ya Upandaji Miti
Milioni 1 mwaka huu wa 2022, pamoja na misaada kwenye mashule na hata Hospitali
zetu, ikiwemo ya Taifa ya Muhimbili ambako tumeingia makubaliano ya kuboresha
Wodi ya Uzazi na tumetumia zaidi ya Sh. Mil. 250," alibainisha na kusema
Dar wametumia zaidi ya Mil. 80 katika elimu.
Kwa niaba ya NMB, Mponzi aliahidi kwamba benki hiyo itaendelea kuwa bega kwa
bega na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua kero na changamoto
zinazokwaza ustawi wa elimu na huduma za afya nchini, huku akiwataka watoa
huduma za bodaboda, bajaji, mama lishe, wauza maduka, wafanyabiashara na
wajasiriamali kufika matawini kupata QR Code zao.
No comments:
Post a Comment