HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 27, 2023

WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU WATAKIWA KUFUATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA UVUNAJI

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema  haijazuia biashara ya mazao ya Misitu huku ikiwataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu  kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kuna kuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha Vijijini Mhe. Michael Costantino Mwakamo, aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).


”Natoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya Misitu wafuate Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa” Mhe. Masanja amesisitiza.


Amesema Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu/miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.



Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Mhe. Agnes Mathew Marwa, kuhusu Serikali kuwatafutia eneo mbadala Wananchi wa Vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitisha uhifadhi Mhe. Masanja amesema kuwa zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo Wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria itakayohusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.


 

Mhe. Masanja amesema kuwa Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika eneo la Virian-Kata ya Stoo ambapo Wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.


Aidha, Halmashauri ya Mji wa Bunda imeandaa mpango wa kutwaa na kulipa fidia maeneo mbadala ya makazi yenye ukubwa wa ekari 1,625 katika maeneo ya Manyamanyama/Bitaraguru; Butakale; na Guta/Nyabehu. Maeneo yote hayo yatapimwa na kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaotoka Kata ya Nyantwari.

No comments:

Post a Comment

Pages