Na Miraji Msala
Dar es Salaam – Sherehe za mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Tegeta A, Halmashauri ya Ubungo, zilihitimishwa kwa ujumbe mzito wa malezi na mshikamano wa kifamilia kutoka kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Angle Park, Bonifasi Daniely.
Akiwa anazungumza mbele ya wazazi, walimu na wanafunzi, Daniely alisema kipindi cha mpito kutoka shule ya msingi kwenda sekondari ni nyeti na kinahitaji uangalizi wa karibu wa familia.
“Watoto wanapomaliza darasa la saba, wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kuathiriwa na marafiki, mitandao ya kijamii au hata changamoto za kiuchumi. Familia ikisimama pamoja katika malezi, mtoto hupata msingi imara wa kimaadili na kielimu,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa jukumu la malezi si la mzazi mmoja, bali ni mshikamano wa familia nzima unaoungwa mkono na shule na jamii.
“Malezi bora ndiyo nguzo ya mafanikio ya elimu. Shule inaweza kutoa maarifa, lakini familia ndiyo msingi wa tabia njema na uadilifu wa mtoto,” aliongeza.
Ili kuonyesha mshikamano wa kweli, Daniely alitangaza msaada wa kuchimba shimo la maji taka lenye thamani ya shilingi milioni 6, akisema lengo ni kuboresha mazingira ya afya na usafi kwa wanafunzi. Hatua hiyo ilishangiliwa na wazazi na pamoja na walimu.
Mahafali hayo yalipambwa na burudani za wanafunzi, ngoma za kitamaduni na michezo ya kuigiza, huku wazazi wakibadilishana mawazo juu ya namna ya kushirikiana zaidi na watoto wao katika kipindi cha mpito kabla ya kuanza kidato cha kwanza.
“Tuwape watoto muda, tuwasikilize na tuwafundishe maadili mema. Sekondari siyo tu darasa jipya, bali ni lango la maisha mapya,” alisisitiza Daniely katika kuhitimisha hotuba yake.
September 14, 2025
Home
Unlabelled
Mahafali Tegeta A: Mgeni Rasmi Asisitiza Malezi na Ushirikiano wa Familia
Mahafali Tegeta A: Mgeni Rasmi Asisitiza Malezi na Ushirikiano wa Familia
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.





No comments:
Post a Comment