MWANARIADHA Mtanzania, Alphonse Felix Simbu, mapema leo Jumatatu Septemba 15, ameibuka na medali ya dhahabu ya Mashindano ya Dunia yanayofanyika Tokyo, Japan baada ya kukimbia marathon ya kinyanganyiro hicho kwa masaa mawili, dakika tisa na sekunde 48 (2:09:48).
Simbu ambaye ni askari mwenye cheo cha Sajenti wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), alilazimika kufanya kazi ya ziada kutwaa Medali ya Dhahabu akimshinda kwa sekunde sifuri nukta 3 (0.03) Mjerumani Amanal Petros aliyechukua Medali ya Fedha.
Iliass Aouani wa Italia, alimaliza kinyang'anyiro akiwa mshindi wa tatu na kutwaa medali ya Shaba, baada ya kutumia masaa mawili, dakika tisa na sekunde 53 (2:09:53).
Baada ya mchuano mkali uliojumuisha pia maili 26 za Mitaa ya Jiji la Tokyo, mbio hizo zilimalizikia kwenye Uwanja wa Taifa wa Japan, ambako shangwe za mashabiki waliojazana dimbani hapo ziliongeza ari na morali ya Simbu mwenye umri wa miaka 33, hivyo kumpiku Petros kwa hatua moja ya mwisho.
Simbu anakuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa Medali ya Dhahabu ya Mashindano ya Dunia, ushindi uliokuja miezi michache tangu atwae Medali ya Fedha ya mbio za Boston Marathon.

Nyota huyo pia aliwahi kutwaa Medali ya Shaba ya Mashindano ya Dunia ya London, Uingereza mwaka 2017 na Medali ya Fedha Mashindano ya Jumuiya ya Madola Mwaka 2022 huko Birmingham, Uingereza.
Pia, Simbu ni mshindi wa Medali ya Fedha ya Mashindano ya Dunia ya Majeshi yaliyofanyika Wuhan, nchini China (CISM 2019)
MATOKEO KWA UFUPI
1. Alphonce Simbu (Tanzania) 2:09:48,
2. Amanal Petros (Ujerumani) 2:09:48,
3. Iliass Aouani (Italia) 2:09:53




No comments:
Post a Comment