HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 10, 2025

Mbeto: Tuliahidi, tunaenda kuwaonyesha

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati anazindua soko la kisasa na stendi Chuini, Wilaya ya Magharibi ‘A’, alisema wakati wa kampeni 2020, alipita kuzungumza na wafanyabishara waliopo pembeni mwa barabara.

Walimwambia kuwa changamoto yao kubwa ni soko kwa ajili ya kufanyiabiashara, mikopo ya biashara na unafuu wa kodi katika masoko na akaahidi kuwa iwapo atapata ridhaa yao kuwa Rais basi angeyatimiza matakwa yao hayo na siku hiyo alienda kutimiza ahadi yake kwa wafanyabiashara hao.


Dkt. Mwinyi anaenda Chuini kuwakabidhi soko ambaloaliwahidi na upande mwingine akiwa katika kampeni zake hizo 2020, anakutana na wananchi mitaani alikowatembelea kuomba kura na mmojawapo anamuambia kuwa watu wako hatuwaoni, hatujui nani tumueleze shida zetu.

Hilo analichukua Dkt. Mwinyi na wakati analichakata wanatokea vijana wanamueleza kuwa wamebuni APP ambayo itamuwezesha kuwasiliana na wananchi wake moja kwa moja ambayo ikapewa jina la ‘Sema na Rais-Mwinyi’.

Anapata faraja na vijana wanaiboresha zaidi na kufanya watu kuweza kupiga simu na kuzungumza na Rais na wasaidizi wake na hata kutuma meseji za kawaida kwenye ‘Viswaswadu’ kueleza changamoto zao na kikubwa zaidi, anaingiza timu ya vijana mitaani kuelimisha umma jinsi ya kutumia mfumo huo.

Ahadi hiyo ni moja kati ya ahadi lukuki alizotoa kwa waZanzibari ambazo kulingana na Ilani ya CCM 2020/2025, ameitimiliza kwa zaidi ya asilimia 100 katika sekta zote na siri kubwa ya mafanikio hayo anasema Dkt. Mwinyi ni kutokana na kuwepo kwa amani na wananchi kuwa na umoja baina yao jambo ambalo anaomba liendelee 2025/2030.

Mtindo alioutumia wakati wa kampeni umekuwa na matokeo chanya ambayo yanaonekana leo Zanzibar kuanzia miundombinu ya barabara, hospitali zilizojengwa kila wilaya, viwanja vya michezo, malipo kwa wazee, huduma za afya, ujenzi viwanja vya ndege, masoko, maeneo ya uwekezaji, bandari za Fumba na Mangapwani.

Madaraja, barabara za juu kupunguza msongamano, matumizi ya Tehama katika ufundishaji kuanzia shule za msingi, mikopo ya asilimia 10 kwa wajasiriamali, Hatifungani za Sukuk, mazingira mazuri ya uwekezaji, miradi mikubwa ya maji na umeme, nyumba bora za makazi kwa waliopisha miradi ya kimakakati.

Nyumba za madaktari za kisasa zenye kila kitu ndani kuanzia sufuria za kupikia hadi mashine za kufulia na luninga kubwa za ukutani, makazi bora ya kisasa kwa wazee na mahitaji yote muhimu, chakula kwa wagonjwa kinachotolewa kwa wanaolazwa kulingana na ushauri wa daktari na ajira kwa vijana kupitia uwekezaji unaofanyika. 

Mambo ni mengi ambayo yamefanyika Zanzibar kuanzia Unguja hadi Pemba na hivi karibuni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis anasema wanachoenda kufanya kwenye kampeni zao ambazo zitazinduliwa rasmi Jumamosi 13 Septemba 2025 ni kuwaonyesha kile ambacho kimefanyika.

Ingawa hajaeleza iwapo mikutano ya hadhara na siasa za majukwaani zitakuwepo au la lakini ukweli upo wazi kuwa kuna kazi kubwa imefanywa Rais Dkt. Hussein Mwinyi na pengine kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya CCM, atafanya kama kampeni za 2020 kwa kuwatembelea wananchi na kuzungumza nao au anakuja na stahili mpya katika kampeni zake katika uchaguzi mkuu 2025?




No comments:

Post a Comment

Pages