HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 15, 2025

Simbu: Najivunia rekodi kuwa Mtanzania wa Kwanza Bingwa wa Dunia


BINGWA wa Dunia wa mbio ndefu za Mashindano ya Riadha ya Dunia (World Athletics Championship - WAC 2025), Alphonce Felix Simbu, amesema moja ya ndoto zake ilikuwa ni kutwaa taji hilo na kwamba anajivunia rekodi ya kuwa Mtanzania wa Kwanza kufikia mafanikio hayo. 

‎Simbu ametikisa Dunia asubuhi ya leo Jumatatu Septemba 15, baada ya kumbwaga Mjerumani Amanal Petros kwa sekunde sifuri nukta tatu (0.03), wote wakikimbia kwa masaa mawili, dakika tisa na sekunde arobaini na nane (2:09.48).

‎Iliass Aouani wa Italia, alimaliza kinyang'anyiro hicho akiwa mshindi wa tatu na kutwaa medali ya Shaba, baada ya kutumia masaa mawili, dakika tisa na sekunde 53 (2:09:53).
‎ 

‎Akizungumza baada ya ushindi huo, Simbu amesema: "Kwakweli ninajisikia furaha sana, kuandika historia hii ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa Medali ya Dhahabu ya Mashindano ya Dunia, haikuwahi kutokea Mtanzania kabla yangu kufanya hivyo.

‎"Nashukuru leo nimefanikiwa kuweka rekodi hii, na nikiri kwamba ubingwa wa Dunia ilikuwa moja ya ndoto zangu na nafurahi kwamba hatimaye nimetimiza," amesema Simbu ambaye pia ni askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha Sajenti.

‎Ushindi wa Simbu katika Mashindano ya Dunia, umekuja miezi michache tangu atwae Medali ya Fedha ya mbio za Boston Marathon. 

‎Nyota huyo pia aliwahi kutwaa Medali ya  Shaba ya Mashindano ya Dunia ya London, Uingereza mwaka 2017 na Medali ya Fedha Mashindano ya Jumuiya ya Madola Mwaka 2022 huko Birmingham, Uingereza. 

‎Pia, Simbu ni mshindi wa Medali ya Fedha ya Mashindano ya Dunia ya Majeshi yaliyofanyika Wuhan, nchini China (CISM 2019)


No comments:

Post a Comment

Pages