HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 09, 2025

Taifa Stars dimbani leo, ugumu wa kuwa 'best looser' uko hapa ‎

KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', kinashuka dimbani New Amaan Complex, Zanzibar, kuwavaa Niger, katika mechi ya Kundi E kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, huku ikikabiliwa na mtihani mzito zaidi inapowania moja ya nafasi nne za 'best loosers' ili kucheza mechi za mtoano.

‎Taifa Stars inayonolewa na Hemed Suleiman 'Morocco', inacheza na Niger saa 10 alasiri ikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Congo-Brazzaille (Septemba 5), katika siku ambayo Morocco iliichapa Niger na kufuzu moja kwa moja fainali za mwakani zinazoandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Canada, Marekani na Mexico. 

‎Baada ya Morocco kuwa timu ya kwanza Afrika kufuzu fainali hizo, tumaini pekee la Taifa Stars limebaki kuwa ni kumaliza katika nafasi nne za juu za msimamo wa timu zitakazomaliza kwenye nafasi ya pili ya makundi yao, zikiwa na matokeo bora 'best loosers.' 

‎Wengi miongoni mwa Watanzania wanadhani inaweza kuwa rahisi kwa Taifa Stars kuingia katika orodha ya timu nne za juu kwenye msimamo wa Washindwa Bora hao, lakini ukweli na uhalisia ni kuwa, huko nako ni kugumu mno kwa Stars 'kutoboa' kucheza mechi za mtoano.

‎Kufikia leo inapoivaa Niger, Tanzania inashika nafasi ya tisa ya msimamo wa 'best loosers' ikiwa na pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara sita.

‎Na iwapo itashinda leo dhidi ya Niger na Kisha kuichapa Zambia hapo Oktoba, itafikisha alama 16 tu, ambazo kuna timu zaidi ya sita itaweza kuzivuka kutokana na pointi zao za sasa na idadi ya mechi zilizosalia.

‎Msimamo wa 'best loosers' kwa sasa unaongozwa na Gabon, inayoshika nafasi ya pili Kundi F ikiwa na alama 18, ikiwa na mechi tatu mkononi. 

‎Timu ya pili ni Madagascar, yenye pointi 16 na salio la mechi mbili mkononi kundi I. 'Simba Wasioshindika' Cameroon wana pointi 15 katika kundi D, wakiwa na mechi tatu mkononi. 

‎'Simba wa Teranga' Senegal wanaoshika nafasi ya pili Kundi B, wameshajikusanyia alama 15 na salio la mechi tatu mkononi, huku Uganda nao wakiwa na pointi 15 katika Kundi G ilikobakisha mechi mbili baada ya kushuka dimbani mara nane.

‎Burkina Faso wenye alama 14 baada ya mechi saba za Kundi A, wanawania kuingia 'top four' wakiwa na mechi tatu. 

‎Hii ina maana kuwa, wakati Taifa Stars ikipambana kuvuna alama sita zote katika mechi mbili zilizosalia ili kupata nafasi yaa 'best loosers', Madagascar wao wanasaka alama moja kuwa juu ya Tanzania, huku Cameroon wakitafuta alama mbili katika mechi tatu, kama ilivyo kwa Senegal. 

‎Uganda 'The Cranes,' na wenyewe wanapambana kushinda mechi mbili zilizobaki ili kuingia 'best loosers', kama ilivyo kwa Burkina Faso ambayo Ina alama 14 na mechi tatu mkononi. Je, umeuona ugumu wa Tanzania kupata moja kati ya nafasi nne za juu ili kuingia mechi za mtoano?


No comments:

Post a Comment

Pages