MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Young Africans 'Yanga,' leo Alhamisi September 11, wameingia mkataba na Kampuni ya BlackBirds ya Uholanzi, kwa ajili ya Teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - Al).
Kwa mujibu wa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, mfumo huo ni kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa za ufanisi wa wachezaji wa klabu yake, ambayo imeingia kwenye rekodi ya kuwa ya kwanza Afrika kuingia kwenye mkataba huo wa kimfumo.
Hafla ya kusaini mkataba huo usio na thamani ya pesa taslimu, imefanyika Makao Makuu ya Yanga, yaliyopo katika makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, ambapo Blackbirds imewakilishwa na Thim van der Wejden na Waalgard.
Akizungumza na wanahabari wakati wa hafla hiyo, Injinia Hersi alisisitiza kuwa makubaliano hayo yanaifanya Yanga kuwa klabu ya kwanza Afrika kutumia mfumo wa kisasa wa aina hiyo, ambao pia utasaidia kusoma ufanisi, ubora na udhaifu wa wapinzani wao.
"Mfumo huu wa Akili Mnemba utasaidia kukusanya na kuchambua taarifa za wachezaji wetu. Ni fahari kubwa kusema Yanga ndiyo klabu ya kwanza Afrika kuingia kwenye ushirikiano wa aina hii inayoendana na kasi ya Teknolojia duniani,” alisema Hersi.
Kwa upande wake, Thim van der Weijden, alisema, kuichagua Yanga haikuja kwa bahati nasibu, bali ni matokeo ya kuvutiwa na ukubwa wa klabu hiyo pamoja na mchakato wa mabadiliko uliofanywa na mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania.
“Tumechagua Yanga kwa sababu ni moja ya klabu kubwa Afrika, na zaidi ni mvuto uliomo katika mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hii. Sisi Blackbirds tunaamini mfumo huu utachangia ufanisi wa kuipeleka Yanga mbele kulingana na mahitaji ya teknolojia,” alisisisitiza Van der Weijden.


No comments:
Post a Comment